Mageuzi ya Sekta ya Afya:Nafasi ya MSD katika kuboresha huduma za matibabu nchini Tanzania

NA GODFREY NNKO

SEKTA ya Afya nchini Tanzania imeendelea kushuhudia mageuzi makubwa katika miaka ya hivi karibuni, yakichochewa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji wa Serikali pamoja na maboresho ya mifumo ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Miongoni mwa taasisi zilizo mstari wa mbele katika mabadiliko hayo ni Bohari ya Dawa (MSD), ambayo imeendelea kuwa mhimili muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya afya.

Akizungumza katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika katika Ofisi za MSD Kanda ya Kati Kizota mkoani Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Mavere Tukai amesema, taasisi hiyo ina jukumu la msingi la kuhakikisha bidhaa zote muhimu za afya zinapatikana kwa wakati, kwa ubora unaokidhi viwango, na kwa gharama nafuu kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa,uwepo wa bidhaa za afya ni mhimili muhimu wa utoaji wa huduma bora za afya, akibainisha kuwa kukosekana kwa bidhaa hizo huathiri moja kwa moja ufanisi wa sekta hiyo.

“Bila uwepo wa bidhaa za afya, sekta ya afya haiwezi kukamilika. Tunahakikisha bidhaa zote zinakuwa salama, zenye ubora unaotakiwa na zinawafikia wananchi kwa wakati,”amefafanua Bw. Tukai.

Aidha, ameeleza kuwa,MSD inaendelea kuwa kiungo muhimu kati ya wazalishaji na vituo vya kutolea huduma za afya, ambavyo humgusa mwananchi moja kwa moja kupitia mifumo mbalimbali ya utoaji huduma nchini.

Kwa mujibu wa Bw. Tukai, majukumu makuu ya MSD yanajumuisha uzalishaji, ununuzi, uhifadhi katika maghala, pamoja na usambazaji wa bidhaa za afya kwa wateja.

Ameongeza kuwa, MSD ndiyo msambazaji mkuu wa bidhaa za afya katika vituo vya umma, ikihudumia kati ya asilimia 81 hadi 83 ya mahitaji yote, huku sehemu iliyobaki ikikamilishwa na washirika katika ngazi za mikoa.
Katika hatua nyingine, Bw. Tukai amebainisha mafanikio yaliyopatikana katika kuboresha upatikanaji wa bidhaa hizo, akieleza kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano, kiwango cha utimilifu wa bidhaa za afya kimeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka asilimia 40 hadi zaidi ya asilimia 80 kwa sasa.

Pia, wahariri na waandishi wa habari walipata fursa ya kutembelea Hospitali ya Jiji la Dodoma pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida ili kujionea hali halisi ya utoaji huduma za afya na mchango wa MSD katika kuboresha sekta hiyo.

Ziara hiyo ilitoa taswira halisi ya maendeleo yaliyofikiwa pamoja na changamoto zinazohitaji kuangaliwa ili kuimarisha zaidi huduma hizo.

Hospitali ya Jiji Dodoma

Katika Hospitali ya Jiji la Dodoma, imebainika kuwa licha ya kuwa hospitali hiyo ni mpya, tayari imefanikiwa kutoa huduma mbalimbali za matibabu kwa ufanisi mkubwa.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo,Dkt.Joshua Mwalongo ameeleza kuwa uwekezaji wa Serikali umeiwezesha hospitali kuwa na miundombinu na vifaa tiba vya kisasa vinavyokidhi mahitaji ya wananchi.
Amesisitiza kuwa, MSD imekuwa daraja muhimu katika kufanikisha maono ya Serikali ya kuboresha sekta ya afya, kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya katika hospitali hiyo, zaidi ya asilimia 92 ya dawa muhimu zinapatikana, hali inayochangia kupunguza adha kwa wagonjwa.

Aidha, Mfamasia Margret Mhalule ameipongeza Serikali kwa kuongeza bajeti ya dawa, jambo lililoiwezesha MSD kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Mhaule ameeleza kuwa,usambazaji wa dawa umeimarika kwa kiasi kikubwa, na hivyo kupunguza changamoto za awali za upungufu wa dawa katika vituo vya afya.

Manyoni

Kwa upande wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, mafanikio yaliyopatikana yanaonesha wazi mchango wa MSD katika kuboresha huduma za afya vijijini.

Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt. Bwire Robert amebainisha kuwa mageuzi ya kidijitali yaliyotekelezwa na MSD yamerahisisha mchakato wa kuagiza dawa na vifaa tiba, kuanzia ngazi ya kijiji hadi hospitali za wilaya.
Ameeleza kuwa, mfumo huo umeongeza uwazi, kasi, na ufanisi katika upatikanaji wa bidhaa za afya, huku ukipunguza malalamiko ya wananchi kuhusu ucheleweshaji wa huduma.

Kwa sasa, vituo vya afya vina uwezo wa kuagiza dawa na kuzipokea ndani ya muda mfupi, jambo linaloimarisha utoaji wa huduma kwa wakati.

Vifaa tiba vya kisasa

Uwekezaji katika vifaa tiba vya kisasa umeleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma, hususan katika maeneo ya huduma maalum kama vile uangalizi wa watoto njiti.

Hospitali ya Manyoni imefanikiwa kuanzisha chumba maalum cha kuhudumia watoto wachanga njiti, kikiwa na vifaa vya kisasa vilivyotolewa kupitia MSD.

Kwa mujibu wa Dkt.Bwire, uwepo wa vifaa hivyo umechangia kupunguza vifo vya watoto njiti kwa zaidi ya asilimia 90, mafanikio ambayo yanaonesha athari chanya ya uwekezaji huo.
Aidha, hospitali hiyo sasa ina uwezo wa kuhudumia hata watoto wenye uzito mdogo sana, jambo ambalo hapo awali lilikuwa changamoto kubwa.

Vilevile, hospitali imeboresha huduma za maabara kwa kutumia mashine za kisasa zikiwemo za kupima sampuli nyingi kwa wakati mmoja, vifaa vya uchunguzi wa mionzi (Ultrasound), pamoja na mashine za upasuaji na usingizi. Maboresho haya yamepunguza msongamano wa wagonjwa na kuongeza ubora wa huduma.

Mafanikio ya MSD

Katika ngazi ya kitaifa, MSD imeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka minne kuanzia 2021/22 hadi 2024/25.

Mapato ya taasisi hiyo yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 100, kutoka shilingi bilioni 315 hadi kufikia zaidi ya shilingi bilioni 640.
Aidha, upatikanaji wa bidhaa za afya umeongezeka kutoka asilimia 42 hadi kufikia asilimia 73 kufikia Machi 2026.

Hali kadhalika, kiwango cha utimizaji wa mahitaji ya vituo vya afya kimeongezeka hadi asilimia 77, hatua inayodhihirisha kuimarika kwa mfumo wa usambazaji.

Mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa mizunguko ya usambazaji kutoka mara nne hadi sita kwa mwaka, usambazaji wa mashine za kusafisha damu (dialysis), pamoja na ujenzi wa maghala ya kisasa katika kanda mbalimbali nchini.

Licha ya mafanikio hayo, bado kuna changamoto zinazoikabili MSD, ikiwemo uhaba wa mtaji wa kutosha kununua bidhaa za afya kwa kiwango kinachohitajika, ucheleweshaji wa bidhaa kutoka kwa wasambazaji, pamoja na uhaba wa miundombinu ya kutosha ya kuhifadhi bidhaa hizo.
Aidha, utegemezi mkubwa wa uagizaji wa bidhaa za afya kutoka nje ya nchi unaendelea kuwa changamoto, kutokana na uwezo mdogo wa viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa hizo kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya taifa.

Kwa ujumla, mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya yanaonesha wazi kuwa uwekezaji wa Serikali pamoja na maboresho ya kiutendaji ya MSD yameleta mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za afya nchini.

Aidha,kuimarika kwa upatikanaji wa dawa, vifaa tiba vya kisasa, na mifumo ya kidijitali ni hatua muhimu kuelekea huduma bora na jumuishi kwa wananchi wote.

Hata hivyo, kuna haja ya kuendelea kuwekeza zaidi katika miundombinu, rasilimali fedha, na uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya ili kuhakikisha mafanikio haya yanadumu na kuongezeka kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here