Wizara ya Madini yalenga mageuzi makubwa kupitia bajeti ya 2026/2027

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Madini imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 174.98 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu yake pamoja na kufikia lengo la ukusanyaji wa maduhuli unaotarajiwa kuzidi shilingi trilioni 1.4.
Akiwasilisha makadirio hayo bungeni jijini Dodoma leo Aprili 27,2026 Waziri wa Madini, Mhe.Anthony Peter Mavunde amesema, fedha hizo zitawezesha wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake kuendelea kusimamia sekta ya madini kwa ufanisi zaidi, sambamba na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Amefafanua kuwa,kati ya fedha zilizoombwa, shilingi bilioni 71.51 sawa na asilimia 40.87 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayolenga kukuza sekta ya madini na kuongeza thamani ya rasilimali hizo nchini.
Pia, shilingi bilioni 103.47 sawa na asilimia 59.13 zitatumika kwa matumizi ya kawaida, ikiwa ni pamoja na kugharamia shughuli za uendeshaji wa wizara na taasisi zake.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, ndani ya bajeti ya matumizi ya kawaida, shilingi bilioni 27.36 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, huku shilingi bilioni 76.11 zikielekezwa katika matumizi mengineyo ya kiutendaji.

Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa,utekelezaji wa bajeti hiyo utaimarisha ukusanyaji wa maduhuli unaolengwa kufikia shilingi trilioni 1.406, pamoja na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali madini.

Ameongeza kuwa,wizara itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, kuendeleza mnyororo wa thamani wa madini, na kuongeza ajira kwa Watanzania kupitia miradi ya kimkakati.
Waziri Mavunde ameeleza kuwa,kupitishwa kwa bajeti hiyo kutatoa fursa zaidi kwa sekta ya madini kukua na kuwa chanzo kikuu cha mapato ya Serikali pamoja na fedha za kigeni.

Aidha, Serikali imejipanga kuhakikisha fedha zitakazoidhinishwa zinatumika kwa uwajibikaji na ufanisi ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Amesema kwa mujibu wa utafiti wa taasisi ya Fraser ya Canada wa mwaka 2025, Tanzania ilishika nafasi ya nne Afrika na ya 34 duniani katika kiashiria cha kuvutia uwekezaji, huku ikipata alama 68.04 mwaka 2025 ikilinganishwa na 62.75 mwaka 2024.

Amebainisha pia kuwa,Tanzania ipo nafasi ya 15 duniani kwa wingi wa rasilimali madini ikiwa na alama 75, hali inayoonyesha uwezo mkubwa wa sekta hiyo katika kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 2025, sekta ya madini imeendelea kuongoza kwa kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI), ambapo mtaji ulifikia dola za Marekani bilioni 9.79 mwaka 2024 kutoka dola bilioni 9.15 mwaka 2023 na dola bilioni 8.64 mwaka 2022.

Ongezeko hilo limechangiwa na mazingira wezeshi ya uwekezaji, upanuzi wa miradi iliyopo pamoja na uwekezaji wa faida zinazozalishwa ndani ya sekta.

Aidha, Serikali imepiga hatua katika kuendeleza madini muhimu na mkakati kwa kuingia mikataba ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya niobium, nikeli, kinywe na dhahabu.

Mfano ni kusainiwa kwa mkataba wa mradi wa uchimbaji wa madini ya niobium wa Panda Hill mkoani Mbeya tarehe 24 Machi,2026.

Mradi huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa barani Afrika na kuiweka Tanzania katika nafasi ya wazalishaji wakubwa wa madini hayo duniani.
Unakadiriwa kuzalisha ajira 1,600 za moja kwa moja na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 6,000, pamoja na kuchochea matumizi ya ndani ya takribani dola za Marekani bilioni 1.77.

Serikali pia inatarajia kupata mapato ya takribani shilingi trilioni 2 kupitia mrabaha, kodi, tozo na gawio la hisa zake.

Kuhusu mwenendo wa soko la madini duniani, Waziri Mavunde amesema,bei ya dhahabu imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, ikifikia wastani wa dola 4,190.47 kwa wakia kutoka dola 2,655.80 kwa kipindi kama hicho mwaka uliotangulia, hali inayochangiwa na mahitaji makubwa ya dhahabu kama hifadhi salama ya thamani.

Hata hivyo, ameeleza kuwa,baadhi ya madini yamekabiliwa na kushuka kwa bei, ikiwemo almasi iliyopungua kwa asilimia 5.39 kutokana na ushindani wa almasi za viwandani, pamoja na makaa ya mawe yaliyoshuka kwa asilimia 34.50 kufuatia kupungua kwa mahitaji ya soko la dunia.
Upande wa madini ya Tanzanite amesema, soko lake limeendelea kukabiliwa na changamoto ya uhakika wa masoko, hali iliyosababisha kushuka kwa bei kwa asilimia 6.72 katika kipindi husika.

Kwa ujumla, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa, ongezeko la mahitaji ya madini mkakati kama lithium, cobalt na nickel katika teknolojia za kisasa na nishati safi linaipa Tanzania fursa ya kuongeza thamani ya madini hayo ndani ya nchi, kukuza ajira na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here