NA DIRAMAKINI
MAHAKAMA ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya imemhukumu kifungo cha miaka 60 jela mwandishi wa habari na mtangazaji wa redio, Zawadi Jackson Mwakijolo, baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.
Hukumu hiyo imetolewa Aprili 29, 2026 na Hakimu Mkazi,Mhe. Paul Mabula Barnabas, kufuatia ushahidi uliowasilishwa mahakamani kuthibitisha bila shaka kwamba mshitakiwa alihusika na usafirishaji wa bangi yenye uzito wa kilo 155.84, iliyokuwa imehifadhiwa katika vifurushi 142.
Kwa mujibu wa taarifa za upande wa mashtaka, Mwakijolo, ambaye ni mkazi wa Itunge Wilaya ya Kyela, alitenda kosa hilo Februari 2, 2025, alipokamatwa na vyombo vya dola akiwa anasafirisha dawa hizo haramu kupitia kivuko kisicho rasmi kinachofahamika kwa jina la January.
Ilielezwa kuwa, lengo la usafirishaji huo lilikuwa ni kusambaza dawa hizo katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya biashara haramu.
Mahakama iliridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, na hivyo kumtia hatiani mshitakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Katika uamuzi wake, mahakama ilisisitiza umuhimu wa kuendelea kukabiliana vikali na vitendo vya usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya vinavyohatarisha ustawi wa jamii.
Hukumu hiyo inatajwa kuwa ni sehemu ya juhudi za mamlaka za kisheria nchini kuhakikisha wahusika wa vitendo vya dawa za kulevya wanachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni njia ya kudhibiti ongezeko la biashara hiyo haramu.
