KILIMANJARO-Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki,Mhe. James Millya, ametembelea Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Holili mkoani Kilimanjaro, kwa lengo la kukagua utoaji huduma na kusikiliza changamoto za wadau.
Akiwa katika ziara hiyo, Mhe.Naibu Waziri amepata maelezo kutoka kwa watendaji wa kituo kuhusu namna huduma zinavyoratibiwa chini ya mfumo wa Himaya Moja ya Forodha unaojumuisha taasisi mbalimbali.
Meneja Mfawidhi wa Forodha wa Kituo cha Holili, Bw. Leornad Mapunda amesema kuwa kituo hicho kimeendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya kisasa inayosaidia kupunguza muda wa kusubiri kwa wasafiri na wafanyabiashara.
Amebainisha kuwa ushirikiano mzuri kati ya taasisi zinazofanya kazi katika kituo hicho umechangia kuongeza ufanisi, ingawa bado kuna changamoto chache za miundombinu , ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kudhibiti magendo na ongezeko la watumiaji wa huduma.
Aidha, aliongeza kuwa juhudi zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa zaidi na kukidhi mahitaji ya biashara inayokua kwa kasi katika mpaka huo.
Mhe.Naibu Waziri baada ya kupokea taarifa hiyo na kukagua miundombinu ya kituo hicho alipata fursa ya kuzungumza na watendaji pamoja na wafanyabiashara wa Mpaka Huo.
Katika hotuba yake, Mhe.Milya amewataka watendaji kuongeza uwajibikaji,kupunguza urasimu na kutumia mifumo ya kidijitar ili kuharakisha utoaji huduma.
















