MBEYA-Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi kwa wananchi katika Tamasha la Kilimo linalofanyika katika viwanja vya Iwambi, mkoani Mbeya.
Akizungumza wakati wa tamasha hilo, Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Ramadhani Mganga, amesema kuwa lengo la ushiriki wao ni kuwahamasisha wananchi kutumia nishati safi na salama kwa kupikia ili kulinda afya zao na mazingira.
Ameeleza kuwa REA inaendelea kusambaza na kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbalimbali za nishati safi ikiwemo majiko ya umeme, majiko ya gesi pamoja na majiko banifu, ambayo yanasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
“Ni muhimu kwa wananchi kuelewa faida za nishati safi, si tu katika kulinda mazingira bali pia katika kuboresha afya kwa kupunguza athari za moshi unaotokana na nishati zisizo salama,”amesema Mganga.
Aidha, amebainisha kuwa kupitia miradi mbalimbali inayoendelea, upatikanaji wa umeme vijijini umeimarika kwa kiwango kikubwa, hatua inayowezesha wananchi wengi zaidi kuanza kutumia nishati safi majumbani.
Wananchi waliofika katika banda la REA wamepata fursa ya kujifunza matumizi sahihi ya majiko hayo pamoja na kupata maelezo kuhusu namna ya kuyapata kwa bei nafuu kupitia miradi ya ruzuku inayoendelea nchini.
Tamasha hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta ya kilimo na nishati, huku likitoa nafasi kwa taasisi mbalimbali kuelimisha umma kuhusu huduma na bidhaa wanazotoa.
















