DODOMA-Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amefungua kikao cha wataalamu wa Wizara hiyo pamoja na ujumbe kutoka Jamhuri ya Korea, ukiongozwa na wataalamu kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Korea (KOICA), kwa lengo la kujadili maandalizi ya Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Majitaka kwa kutumia mifumo ya kisasa, rafiki kwa mazingira na inayozingatia mabadiliko ya tabianchi.
Wakati wa ufunguzi wa kikao jijini Dodoma, Mhandisi Mwajuma amewataka wataalamu wa Wizara ya Maji kutumia fursa hiyo kujadiliana kwa kina na wenzao kutoka Korea ili kubaini manufaa ya mradi huo kwa wananchi, pamoja na kuhakikisha kuwa utekelezaji wake unalinda mazingira na kuchangia kufanikisha maono ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
“Tumeendesha majadiliano kwa takribani wiki mbili na wataalamu hawa kutoka Korea. Ni matarajio yangu kuwa kikao hiki kitazaa matokeo yenye tija kwa nchi yetu. Tunaamini kuwa kupitia ushirikiano huu, tutapata mafanikio katika kuboresha usimamizi wa majitaka na hivyo kuleta manufaa kwa wananchi,” amesema Mhandisi Mwajuma.
Katika kikao hicho, wataalamu wamejadili kwa kina matumizi ya mifumo ya Climate Smart-DEWATS (Decentralized Wastewater Treatment Systems), ambayo inalenga kuboresha usimamizi wa majitaka katika ngazi ya jamii kwa ufanisi na uendelevu.
Mifumo hii ina sifa ya gharama nafuu katika ujenzi na uendeshaji, matumizi madogo ya nishati, pamoja na urahisi wa uendeshaji na matengenezo.
Aidha, mifumo hiyo inawezesha uzalishaji wa nishati mbadala kupitia biogas, urejelezaji wa mabaki ya majitaka (sludge) kuwa mbolea, pamoja na matumizi ya maji yaliyotibiwa kwa shughuli za kilimo.
Hali hii inaimarisha dhana ya uchumi mzunguko (circular economy) kwa kutumia rasilimali kwa ufanisi zaidi na kupunguza athari kwa mazingira.
Pamoja na majadiliano hayo, wataalamu kutoka KOICA wameendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa Wizara ya Maji kwa kuwapatia uzoefu na ujuzi kuhusu utekelezaji wa miradi ya usimamizi wa majitaka iliyofanikiwa katika nchi mbalimbali.




