NA GODFREY NNKO
MAGEUZI makubwa yanayoendelea kushuhudiwa katika sekta ya afya nchini yameanza kuzaa matunda, huku Bohari ya Dawa (MSD) ikitajwa kuwa mhimili muhimu katika kuhakikisha huduma bora za vifaa tiba na dawa zinavifikia vituo vya afya ili kuwahudumia wananchi kwa wakati na kwa ufanisi.
Hali hiyo imebainika hivi karibuni kufuatia ziara ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea Hospitali ya Jiji la Dodoma pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Aidha, katika ziara hiyo, wahariri hao walijionea namna uwekezaji wa Serikali ulivyobadili taswira ya utoaji huduma za afya.
Katika Hospitali ya Jiji Dodoma, licha ya kuwa ni miongoni mwa hospitali mpya nchini, tayari imefanikiwa kutoa huduma mbalimbali za kibingwa na za kawaida kwa wananchi.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt.Joshua Mwalongo amesema, mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali pamoja na ushirikiano wa karibu na MSD.
Ameeleza kuwa,upatikanaji wa dawa muhimu umefikia zaidi ya asilimia 92, hali inayopunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya wagonjwa kukosa huduma.
“MSD imekuwa daraja muhimu la utekelezaji wa maono ya Serikali katika kuboresha sekta ya afya,” amesema Dkt.Mwalongo huku akiipongeza taasisi hiyo kwa kazi kubwa ambayo inafanya kwa ustawi bora wa sekta ya afya nchini.
Mfamasia wa hospitali hiyo, Margret Mhalule ameongeza kuwa,kuongezeka kwa bajeti ya dawa kumeiwezesha MSD kusambaza bidhaa kwa wakati, hatua iliyopunguza malalamiko ya wananchi.
Kwa upande wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, mafanikio makubwa yamechangiwa na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kuagiza na kusambaza dawa pamoja na vifaa tiba.Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Dkt.Bwire Robert amesema,mfumo huo umeongeza kasi ya upatikanaji wa huduma na kupunguza ucheleweshaji uliokuwepo hapo awali.
“Sasa tunaagiza dawa kidijitali kuanzia ngazi ya chini kabisa, na ndani ya muda mfupi tunazipata. Hili limeongeza ufanisi mkubwa katika utoaji huduma."
Moja ya mafanikio makubwa yaliyojitokeza Manyoni ni kuanzishwa kwa huduma maalum za watoto wachanga njiti, kufuatia upatikanaji wa vifaa vya kisasa kupitia MSD.
Kwa mujibu wa Dkt.Bwire, uwekezaji huo umechangia kupunguza vifo vya watoto njiti kwa zaidi ya asilimia 90, huku hospitali sasa ikiwa na uwezo wa kuhudumia hata watoto wenye uzito mdogo sana.
Aidha, huduma za maabara na upasuaji zimeimarika kupitia mashine za kisasa zikiwemo za kupima sampuli nyingi kwa wakati mmoja, vifaa vya uchunguzi wa mimba (Ultrasound), pamoja na mashine za usingizi na upasuaji.Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Manyoni walieleza kuridhishwa na maboresho hayo, wakisema kwa sasa wanapendelea kupata huduma katika hospitali za umma kutokana na uhakika wa dawa na vifaa tiba.
Wamebainisha kuwa,tofauti na ilivyokuwa hapo awali, kwa sasa huduma nyingi zinapatikana bila usumbufu mkubwa.
Awali,Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa amesema kuwa,kanda hiyo kwa sasa inahudumia jumla ya vituo zaidi ya 840 vilivyopo katika mikoa ya Dodoma na Singida, pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.
Huduma hizo zinajumuisha halmashauri 18, zikiwemo nane za Mkoa wa Dodoma, saba za Mkoa wa Singida na moja ya Kiteto.
Amesema, lengo kuu la MSD ni kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa wakati katika vituo vya afya, hatua inayochangia kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa mfumo mzima wa huduma za tiba nchini.
Kwa mujibu wa Bi.Jumaa, MSD Kanda ya Dodoma imeweka utaratibu maalum wa ugawaji wa huduma kwa wateja wake, kwa kuwagawa katika makundi mawili.
Kundi la kwanza linajumuisha Mkoa wa Singida, huku kundi la pili likijumuisha Mkoa wa Dodoma pamoja na Halmashauri ya Kiteto.
Amefafanua kuwa, utoaji wa huduma hufanyika kwa mzunguko wa kila baada ya miezi miwili, ambapo kila kundi hupatiwa huduma kwa awamu tofauti.
Utaratibu huo unawezesha kila kundi kuhudumiwa mara sita kwa mwaka, hivyo kuhakikisha upatikanaji endelevu wa dawa na vifaa tiba katika maeneo husika.
“Kwa mfano, iwapo mwezi Aprili tunahudumia Mkoa wa Dodoma, basi mwezi Mei tunahudumia Mkoa wa Singida. Mfumo huu umetusaidia kufikia vituo vyote kwa ufanisi na kwa wakati,” ameeleza Bi.Jumaa.
Aidha, Meneja huyo amesisitiza kuwa MSD iko tayari kukabiliana na hali za dharura wakati wowote, hususan pale kunapotokea milipuko ya magonjwa au mahitaji ya ghafla ya vifaa tiba.
Kwa ujumla, mafanikio ya MSD yanaashiria mwanzo wa enzi mpya ya huduma za afya nchini, ambapo wananchi wanaanza kupata huduma bora, za uhakika na kwa wakati.















