Zanzibar yadhamiria kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia na usafirishaji haramu wa binadamu

ZANZIBAR-Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto,Mhe. Anna Athanas Paul amesema ni muhimu kwa wananchi kujitokeza kuanzisha asasi zisizo za kiserikali (NGOs) zitakazoshughulikia uanzishwaji wa nyumba salama kwa wahanga wa usafirishaji haramu wa binadamu na manusura wa vitendo vya ukatili na udhalilishaji, ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na ulinzi kwa wahanga hao.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa kupokea ripoti ya utafiti wa mwenendo wa Nyumba Salama uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamiaji (IOM), kikao kimefanyika jana katika ukumbi wa wizara hiyo Kinazini Unguja.

Mhe.Anna amesema,endapo wananchi watajitokezwa kuanzisha nyumba salama kwa matakwa ya Serikali hatua hiyo itaweza kuleta ufanisi na kupunguza changamoto ziliyopo katika utowaji wa huduma kwa wahanga na manusura wanaopolekewa nyumba salama.
"Nyumba salama ni nyumba inayowahifadhi wahanga wa usafirishaji haramu wa binadamu na manusura wa vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ambayo ipo chini wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar,”amesema Waziri huyo.

Pia ameomba shirika hilo kama litaweza kutafuta NGOs itakayoweza kuendesha nyumba salama kwa kuzingatia miongozo ya Serikali katika uanzishaji wa nyumba hiyo.

Hivyo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaahidi kuipa mashirikiano wa dhati.

Aidha,alieleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kuhakikisha malengo ya wizara,kwani ripoti ya utafiti uliyofanya wa kuangalia mwenendo mzima wa uendeshaji nyumba salama itasaidia katika Mpango wa Taifa wa Kupambana na Vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA VAC 2025/2030).

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, ndugu Abeida Rashid ametoa wito kwa wananchi kuacha utamaduni wa kuficha au kusuluhisha matukio ya udhalilishaji katika ngazi ya familia, kwani hatua hiyo inapelekea hatua za kisheria kutotendeka kwa wahalifu na hatimae vitendo viovu kuongezeka katika jamii.

Amesema,mafanikio ya Mpango wa NPA VAC 2025/2030 yatategemea ushirikiano wa jamii kwa kutoa taarifa na kushiriki kikamilifu katika mapambano ya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto. Hivyo ameiomba jamii kubadilika kwa kuacha tabia ya kuficha taarifa kwa kuogopa muhali au kusuluhisha ndani ya familia.
Vile vile amesema, ripoti ya utafiti iliwasilishwa Aprili 22, 2026 kwa wajumbe wa Kamati ya Mpango wa Taifa wa kupambana na Udhalilishaji dhidi ya Wanawake na Watoto na jana tarehe Aprili 24 imewasilishwa katika Kamati ya Uongozi ya Wizara. Hivyo imeleta mwanga mpya katika kuboresha sera, mipango na mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo.

Mapema mshauri mwelekezi wa ripoti ya utafiti wa mwenendo wa nyumba salama, ndugu Nietiwe Mashafi kutoka IOM ameeleza changamoto kuu zilizobainika ni pamoja na ukosefu wa ushirikiano madhubuti kati ya taasisi za Serikali, Mahakama na asasi za kiraia, upungufu wa rasilimali watu na fedha, mazingira yasiyo rafiki kwa wahanga na watoa wa huduma, pamoja na ukosefu wa elimu kwa baadhi ya watoa huduma.
Kwa upande wa wajumbe wa kikao hicho wameweza kutoa maoni yao kwa ajili ya kuboresha ripoti hiyo ikiwemo changamoto ya kuwafuatilia wahanga baada ya kutoka nyumba salama, marekebisho ya sheria ya usafirishaji haramu wa binadamu, maafisa ustawi kutenganisha tawimwi za ajira za utotoni na usafirishaji haramu wa binadamu ili kuweka sawa taarifa za matukio hayo mawili.

Naye Afisa Miradi Msaidizi wa IOM Tanzania (Ofisi ya Zanzibar), Ndugu Sarah Ali Abdalla, amesema Shirika hilo liko tayari kuendelea kushirikiana na Wizara hiyo kwa kutoa msaada wa vifaa endapo Wizara itaomba eneo katika sehemu ya Bandari ya Zanzibar na kujenga ofisi ya Maafisa Ustawi wa Jamii, ili kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa wahanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here