Amani ya Tanzania ni matokeo ya kazi kubwa ya polisi-Rais Dkt.Samia

DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa amani na utulivu uliopo nchini si jambo la bahati mbaya bali ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Polisi kabla ya kuhitimisha Mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi hilo, Kurasini jijini Dar es Salaam, tarehe 28 Mei, 2026.

Rais Samia ameyasema hayo Mei 28, 2026 katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi kozi namba 1, 2025/2026.
Rais Samia alisema kuwa, kulinda usalama wa raia na mali zao ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa kwani bila amani wananchi hawawezi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi na jambo hilo limekuwa likifanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine hivyo wanapaswa kupewa pongezi kutokana na utulivu uliopo.

Alilitaka Jeshi la Polisi kuusimamia vizuri mfumo huo kwa kuwa taarifa nyingi za kiusalama hutokana na wananchi wenyewe, huku akisisitiza kuwa wananchi wakipewa elimu sahihi wataweza kushiriki kikamilifu katika kuzuia na kutoa taarifa za uhalifu kabla madhara hayajatokea.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, alimshukuru Rais Samia kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, akieleza kuwa uwepo wake unaonesha namna Serikali inavyothamini maendeleo ya Jeshi la Polisi na usalama wa Taifa kwa ujumla.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama wakati wimbo wa Taifa ukiimbwa kwenye uwanja wa Chuo cha Taaluma ya Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam, tarehe 28 Mei, 2026.
IGP Wambura alisema Serikali ya Rais Samia imefanya maboresho makubwa ndani ya Jeshi la Polisi kupitia utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya kurekebisha Mifumo ya Haki Jinai iliyoundwa mwaka 2022.

Alieleza kuwa Jeshi hilo limewezeshwa kwa kiwango kikubwa katika maeneo ya miundombinu, vitendea kazi na maslahi ya askari ambapo zaidi ya miradi 320 ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya Polisi imeendelea kutekelezwa sambamba na upatikanaji wa magari ya kioperesheni, pikipiki, boti na ndege kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi.

Naye Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Dkt. Lazaro Mambosasa, alisema jumla ya wahitimu 719 wamehitimu mafunzo hayo, wakiwemo Maafisa 318 na Wakaguzi Wasaidizi 401.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here