NA DIRAMAKINI
KLABU ya Arsenal imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England (England Premier League) msimu wa 2025-26 ikikata kiu ya miaka 22 bila taji la ligi, baada ya matokeo ya sare ya 1-1 kati ya Manchester City na Bournemouth yaliyoihakikishia ubingwa huo.
Manchester City imelazimishwa sare ya 1–1 katika uwanja wa Bournemouth, matokeo yaliyowafanya washindwe kufikia pointi za Arsenal licha ya mechi moja iliyosalia msimu kumalizika.
Matokeo hayo yameifanya Arsenal kuwa vinara wasioweza kufikiwa katika msimamo wa ligi, na hivyo kutangazwa mabingwa rasmi wa England.
Katika mchezo huo, Bournemouth walitangulia kupata bao dakika ya 39 kupitia kwa Junior Kroupi kabla ya Manchester City kusawazisha dakika za lala salama kupitia Erling Haaland, lakini bao hilo halikutosha kubadili hatima ya mbio za ubingwa.
Ubingwa huu ni wa kwanza kwa Arsenal katika kipindi cha miaka 22, tangu walipopitwa na mafanikio ya ligi mwaka 2004.
Mafanikio haya pia yanatajwa kuwa ni matokeo ya uthabiti wa kikosi hicho chini ya kocha Mikel Arteta, ambaye ameijenga timu yenye ushindani mkubwa katika misimu ya hivi karibuni.
Mashabiki wa Arsenal wameanza sherehe kubwa nchini England na maeneo mbalimbali duniani, wakilitaja tukio hilo kama “kurudi kwa utukufu wa The Gunners” baada ya miaka mingi ya kusubiri.
Kwa upande wa Manchester City, matokeo haya yanachukuliwa kama pigo kubwa katika msimu uliokuwa na ushindani mkali, ambapo walihitaji ushindi ili kuendeleza matumaini ya kutetea ubingwa.
Arsenal sasa inasalia na mechi moja ya kufunga msimu dhidi ya Crystal Palace, lakini tayari imehakikisha ubingwa wake wa ligi.
Ikiwa na alama 82, Manchester City wapo nyuma yao kwa alama 77 huku Man United ikiwa nafasi ya tatu kwa alama 68 na nafasi ya nne inashikiliwa na Aston Villa kwa alama 62, wote wamecheza mechi 37 isipokuwa Manchester City ambao wamecheza mechi 36.
