NA DIRAMAKINI
MAKAMU wa Rais wa zamani wa Nigeria, Atiku Abubakar ameitaka Serikali ya Nigeria pamoja na Shirika la Taifa la Mafuta la Nigeria (Nigerian National Petroleum Company Limited) kusitisha mara moja makubaliano ya ushirikiano yaliyoingiwa kati ya shirika hilo na kampuni mbili za China kwa ajili ya ukarabati na uendeshaji wa mitambo ya kusafisha mafuta ya Port Harcourt na Warri.
Katika taarifa iliyotolewa kupitia msemaji wake wa mawasiliano kwa umma, Phrank Shaibu, Makamu huyo ameeleza kuwa, makubaliano hayo yanahatarisha mustakabali wa uchumi wa Nigeria kutokana na kile alichodai kuwa ni ukosefu wa uwazi, weledi na uhalali wa kiufundi wa kampuni zilizochaguliwa kushiriki katika mradi huo mkubwa wa kimkakati.
Makubaliano hayo yanahusisha kampuni za China za Sanjiang Chemical Company Limited pamoja na Xingcheng (Fuzhou) Industrial Park Operation and Management Co. Ltd, ambazo zimeingia mkataba wa kile kilichoelezwa kama “Technical Equity Partnership” na NNPC kwa lengo la kufufua shughuli za mitambo ya kusafisha mafuta ya Port Harcourt na Warri ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikikumbwa na changamoto za uzalishaji na matengenezo.
Atiku amedai kuwa, baada ya serikali kutumia zaidi ya dola bilioni 2.5 katika miradi ya ukarabati wa mitambo hiyo bila mafanikio ya kuridhisha, haikuwa busara kwa taifa hilo kuingia katika makubaliano mapya na kampuni ambazo, kwa mujibu wa tathmini huru, hazina uzoefu wala uwezo wa kuendesha mitambo mikubwa ya kusafisha mafuta ghafi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kampuni ya Sanjiang Chemical inajihusisha zaidi na uzalishaji wa kemikali za petroli, methanoli na bidhaa nyingine zinazotokana na mafuta, lakini hakuna ushahidi wa wazi unaoonesha kuwa kampuni hiyo imewahi kujenga au kuendesha kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta ghafi chenye ukubwa na ugumu kama wa mitambo ya Port Harcourt na Warri.
Aidha, Atiku alihoji uwezo wa kampuni ya Xingcheng (Fuzhou) Industrial Park Operation and Management Co. Ltd akisema taarifa zilizopo zinaonesha kuwa kampuni hiyo ina uzoefu zaidi katika usimamizi wa maeneo ya viwanda na miundombinu kuliko shughuli za uhandisi wa mafuta na usafishaji wa mafuta ghafi.
Makamu huyo wa zamani wa Rais amesema, hatua ya serikali kupuuza kampuni kubwa za kimataifa zenye uzoefu katika sekta ya usafishaji wa mafuta na badala yake kuchagua kampuni ambazo uwezo wake unaibua maswali mengi, inaweza kuigeuza miradi hiyo kuwa mzigo mwingine mkubwa wa kifedha kwa wananchi wa Nigeria.
Aliongeza kuwa, taifa hilo haliwezi kuendelea kushuhudia mabilioni ya fedha yakitumika katika miradi ya ukarabati wa mitambo ya mafuta bila matokeo ya kudumu huku uwajibikaji na uwazi vikikosekana.
Hata hivyo, baadhi ya makundi ya kiraia nchini humo yamejitokeza kuunga mkono makubaliano hayo, yakieleza kuwa ushirikiano kati ya NNPC na kampuni za China unaweza kusaidia kuimarisha usalama wa nishati, kuongeza ajira na kupunguza utegemezi wa Nigeria kwa mafuta yaliyosafishwa kutoka nje ya nchi.
Mitambo ya kusafisha mafuta ya Warri na Port Harcourt ni miongoni mwa miundombinu muhimu ya sekta ya nishati nchini Nigeria, lakini kwa muda mrefu imekuwa ikikumbwa na changamoto za uzalishaji hafifu, hitilafu za kiufundi na gharama kubwa za ukarabati.
Serikali ya Nigeria imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kufufua mitambo hiyo ili kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.(NA)
