NA GODFREY NNKO
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeipitisha bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya jumla ya shilingi trilioni 2.39 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 huku serikali ikiweka mkazo katika utekelezaji wa vipaumbele vitano vikuu vinavyolenga kuboresha ubora wa elimu, kuimarisha mafunzo ya ufundi pamoja na kukuza sayansi, teknolojia na ubunifu nchini.
Bajeti hiyo imepitishwa leo Mei 8,2026 bungeni jijini Dodoma baada ya wabunge kujadili na kuchangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa siku mbili mfululizo kuanzia Mei 7 hadi Mei 8,2026.
Akihitimisha mjadala wa bajeti hiyo bungeni, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amewashukuru wabunge kwa michango yao mbalimbali iliyolenga kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Pia, amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya wizara hiyo.Awali akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo Mei 7, 2026, Profesa Mkenda alisema kati ya fedha zote zilizoombwa, kiasi cha shilingi 2,394,423,829,000 ni kwa ajili ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Fungu 46).
Alieleza kuwa,kati ya fedha hizo, shilingi 697,841,881,000 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, ambapo shilingi 648,082,352,000 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi, huku shilingi 49,759,529,000 zikielekezwa kwenye matumizi mengineyo ya kiutendaji.
Kwa upande wa miradi ya maendeleo, Waziri Mkenda alisema wizara imeomba shilingi 1,696,581,948,000, ambapo kati ya fedha hizo shilingi 1,337,249,000,000 ni fedha za ndani na shilingi 359,332,948,000 zinatarajiwa kutoka kwa washirika wa maendeleo.Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda alisema Wizara kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO (Fungu 18) imeomba kuidhinishiwa shilingi 3,866,993,000 kwa matumizi ya kawaida.
Kati ya fedha hizo, shilingi 1,335,020,000 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi na shilingi 2,531,973,000 zitatumika katika shughuli nyingine za uendeshaji wa tume hiyo.
Vipaumbele vitano vya Wizara
Akizungumzia mwelekeo wa wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Profesa Mkenda alisema serikali imeandaa vipaumbele vyake kwa kuzingatia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, yenye lengo la kuimarisha ubora wa elimu, kuongeza maarifa na kukuza ujuzi kwa wananchi.
Alisema,Serikali itaendelea kuweka mkazo katika maandalizi ya utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na kukuza sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuendana na mahitaji ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.Kwa mujibu wa Waziri huyo, wizara imejikita katika utekelezaji wa vipaumbele vitano vikuu.
Kipaumbele cha kwanza ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, kufanya mapitio ya sheria mbalimbali za elimu, kuandaa miongozo pamoja na kutoa mafunzo kwa wadau wa sekta hiyo.
Kipaumbele cha pili ni kuongeza fursa na kuboresha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya amali, huku cha tatu kikilenga kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu.
Kipaumbele cha nne ni kuongeza fursa na kuboresha ubora wa elimu ya juu, wakati cha tano kikielekezwa katika kuimarisha uwezo wa taifa kwenye tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa lengo la kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Serikali Kufanya Tathmini ya Sera ya Elimu
Profesa Mkenda alisema,Serikali itafanya tathmini ya miaka miwili ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, ambayo ilianza kutekelezwa Januari 2024 na kuzinduliwa rasmi Februari 1, 2025.
Alisema,tathmini hiyo inalenga kubaini mafanikio yaliyofikiwa pamoja na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa sera hiyo ili kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha sekta ya elimu nchini.
Aidha,Serikali itaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa mpango wa elimu ya lazima ya miaka 10, hatua inayotarajiwa kuwezesha wanafunzi wa darasa la sita na la saba kuanza kupokelewa kwa wakati mmoja kuanzia Januari 2028.Kwa mujibu wa Waziri Mkenda, utekelezaji wa mpango huo unasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika maandalizi ya miongozo, upatikanaji wa rasilimali za ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa muhimu pamoja na utoaji wa mafunzo kwa walimu.
Sheria za Elimu kufanyiwa mapitio
Waziri huyo alisema,Serikali itakamilisha mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 ili kuendana na mabadiliko ya sera na mahitaji ya sasa ya sekta ya elimu.
Pia alisema,mapitio yatafanyika katika sheria zinazosimamia taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara hiyo zikiwemo Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) pamoja na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).Alisema,hatua hiyo inalenga kuhakikisha taasisi hizo zinaendana na mabadiliko ya sera, sheria pamoja na makubaliano ya kikanda na kimataifa.
Katika kuimarisha mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu katika maendeleo ya taifa, Profesa Mkenda alisema,serikali itakamilisha mapitio ya Sera ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1996 ili kubaini kama bado inakidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Alisema,mapitio hayo yatawezesha taifa kuwa na sera madhubuti ya kusimamia masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya taifa pamoja na mahitaji ya kikanda na kimataifa.

