Rais Trump aruhusu nyaraka za maelfu ya viumbe vya ajabu angani kutolewa kwa umma kwa ajili ya uchunguzi na tathmini ya wananchi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Marekani, Donald J. Trump, ametangaza kuachiwa kwa sehemu ya kwanza ya nyaraka zinazohusiana na maelfu ya viumbe vya ajabu angani maarufu kama UFO/UAP kwa umma kwa ajili ya uchunguzi na tathmini ya wananchi.
Katika taarifa yake, Trump amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha uwazi wa kiwango cha juu kuhusu taarifa zinazohusiana na maisha ya viumbe wa anga za mbali na vitu visivyotambulika vinavyoonekana angani.

Amesema kuwa, kupitia Idara ya Vita ya Marekani, utawala wake ulitoa maelekezo ya kutambuliwa na kuwekwa wazi kwa nyaraka za serikali pamoja na video zinazohusiana na matukio hayo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakizua mjadala mkubwa duniani.

“Kwa kutimiza ahadi yangu kwa wananchi, Idara ya Vita imetoa sehemu ya kwanza ya mafaili ya UFO/UAP kwa umma kwa ajili ya mapitio na tafiti,”amesema Trump katika taarifa hiyo.

Aidha, amesisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha uwazi kamili na wa kiwango cha juu katika masuala ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakizungukwa na usiri mkubwa ndani ya Serikali ya Marekani.

Trump amewatuhumu viongozi waliomtangulia kwa kushindwa kuweka wazi taarifa hizo kwa wananchi, akidai kuwa tawala zilizopita hazikuwa tayari kutoa ukweli kuhusu matukio hayo ya ajabu yanayoripotiwa kuonekana katika anga mbalimbali duniani.

Kupitia nyaraka na video mpya zilizotolewa, Trump amesema wananchi sasa wana nafasi ya kujionea wenyewe na kutoa hitimisho kuhusu kile kinachoendelea.

“Wananchi sasa wanaweza kuamua wenyewe, nini hasa kinaendelea.’”

Kwa miaka kadhaa, suala la UFO na UAP limeendelea kuvuta hisia za watu duniani, huku baadhi ya wataalamu wa usalama na anga wakitaka serikali mbalimbali kutoa taarifa zaidi kuhusu matukio hayo ambayo mara nyingi hayapati maelezo rasmi.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mjadala mpana kuhusu uwepo wa maisha nje ya sayari ya Dunia pamoja na siri zinazodaiwa kufichwa kwa muda mrefu na mamlaka mbalimbali za serikali.(NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here