Chelsea yamtangaza Xabi Alonso kuwa Kocha Mkuu mpya kwa mkataba wa miaka minne

NA DIRAMAKINI

KLABU ya Chelsea FC imemtangaza rasmi kocha Mhispania Xabi Alonso kuwa kocha mkuu mpya wa kudumu wa kikosi hicho, akichukua nafasi iliyoachwa na Liam Rosenior ambaye alifutwa kazi mwezi uliopita kutokana na matokeo yasiyoridhisha ndani ya klabu hiyo ya London.
Alonso mwenye umri wa miaka 44 amepewa mkataba wa miaka minne utakaomuweka katika dimba la Stamford Bridge hadi Juni mwaka 2030.

Kwa mujibu wa taarifa ya klabu, kocha huyo anatarajiwa kuanza rasmi majukumu yake Julai 1, 2026 huku akirejea kwenye majukumu ya ukocha miezi kadhaa baada ya kuondoka katika klabu ya Real Madrid CF mwezi Januari,mwaka huu.

Uteuzi wa Alonso unaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpya wa Chelsea kurejesha ushindani wake ndani ya Premier League pamoja na michuano ya Ulaya, baada ya misimu kadhaa ya kuyumba kiuchezaji licha ya uwekezaji mkubwa wa wachezaji.

Ingawa alikaa kwa muda mfupi wa miezi nane tu katika benchi la ufundi la Real Madrid, Alonso bado anaendelea kuhesabiwa miongoni mwa makocha vijana wenye uwezo mkubwa zaidi barani Ulaya kutokana na mafanikio yake ya kipekee akiwa na Bayer Leverkusen.

Kocha huyo alipata sifa kubwa duniani baada ya kuiongoza Bayer Leverkusen kutwaa ubingwa wa Bundesliga msimu wa 2023/24 bila kupoteza hata mchezo mmoja, mafanikio yaliyovunja historia katika soka la Ujerumani.

Mbali na ubingwa huo, Alonso alisifiwa kwa falsafa yake ya soka la kushambulia, nidhamu ya kiuchezaji pamoja na uwezo wa kukuza vipaji vya vijana.

Katika maisha yake ya uchezaji, Alonso aliwahi kung’ara katika vilabu vikubwa vya Ulaya ikiwemo Liverpool FC, Real Madrid na FC Bayern Munich ambapo alijijengea heshima kubwa kama mmoja wa viungo bora wa kizazi chake kutokana na uwezo wake wa kupiga pasi sahihi, utulivu na uongozi uwanjani.

Mashabiki wa Chelsea sasa wanatarajia kuona mabadiliko makubwa ndani ya kikosi hicho chini ya Alonso, hasa katika eneo la mbinu na ushindani, huku uongozi wa klabu ukiamini kuwa uzoefu wake wa kimataifa pamoja na falsafa yake ya kisasa ya soka vitairejesha timu hiyo katika kiwango chake cha ubora barani Ulaya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here