NA GODFREY NNKO
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kuimarisha utoaji pamoja na udhibiti wa huduma za hali ya hewa nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi na usalama katika sekta mbalimbali za uchumi, hususan usafiri wa anga.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 13, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa wakati akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Profesa Mbarawa amesema,Serikali imeendelea kuwekeza katika maboresho ya huduma za hali ya hewa ili kuhakikisha sekta ya usafiri wa anga inakuwa salama,ya kisasa na yenye kukidhi viwango vya kimataifa.
Ameeleza kuwa,katika kipindi cha utekelezaji wa miradi hiyo, TMA imefanikiwa kukamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya Mpanda na Pemba.
Amesema,mitambo hiyo itasaidia kuongeza usahihi wa taarifa za hali ya hewa kwa marubani na wadau wa usafiri wa anga, hatua inayotarajiwa kuimarisha usalama wa safari za ndege pamoja na kuongeza ufanisi wa shughuli za usafiri wa anga nchini.
Mbali na hilo, Waziri huyo amesema TMA inaendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya hali ya hewa nchini, ikiwemo maabara maalumu ya uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa (Calibration Center) inayojengwa jijini Dar es Salaam, ambapo ujenzi wa maabara hiyo umefikia asilimia 46.
Amefafanua kuwa,kukamilika kwa maabara hiyo kutasaidia kuongeza uwezo wa ndani wa uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa, kupunguza utegemezi wa huduma hizo kutoka nje ya nchi na kuongeza ubora wa taarifa zinazotolewa kwa watumiaji mbalimbali wa huduma za hali ya hewa.
Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amesema Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 umezingatia nyaraka na miongozo mbalimbali ya maendeleo ya Taifa ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Nne (FYDP IV 2026/27–2030/31), Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2026/27 pamoja na Mpango Mkakati wa Wizara wa Miaka Mitano wa 2026/27–2030/31.
Aidha, amesema Wizara ya Uchukuzi imezingatia pia maelekezo mbalimbali yanayotolewa na viongozi wakuu wa Serikali kwa lengo la kuhakikisha sekta ya uchukuzi inaendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Akieleza vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Profesa Mbarawa amesema, Serikali itaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi na uendeshaji wa Reli ya Kisasa ya SGR, ukarabati na uboreshaji wa reli za MGR na TAZARA, pamoja na kuimarisha huduma za usafiri wa anga nchini.
Vipaumbele vingine ni pamoja na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa meli, kuboresha huduma za hali ya hewa, kuimarisha udhibiti wa ubora na usalama wa huduma za uchukuzi pamoja na kuboresha vyuo vya mafunzo vya kisekta ili kuongeza wataalamu wenye ujuzi na ushindani.
Katika mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Uchukuzi imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 2.87 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 126.04 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, huku Shilingi trilioni 2.74 zikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan katika sekta za reli, bandari na usafiri wa anga ambazo Serikali imeendelea kuzipa kipaumbele kama nguzo muhimu za maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Tags
Bunge la Bajeti
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Sekta ya Uchukuzi
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania
