EWURA yatangaza bei mpya za mafuta Mei 2026,yatoa sababu ya ongezeko la gharama

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo mpya za bidhaa za mafuta ya petroli zilizoanza kutumika rasmi kuanzia saa 6:01 usiku wa kuamkia Jumatano ya Mei 6,2026, huku ikieleza kuwa mabadiliko hayo yamechochewa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la bei katika soko la dunia pamoja na athari za mivutano ya kisiasa katika Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, EWURA imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kisheria kwa kufuatilia mwenendo wa bei za mafuta kimataifa na kupanga bei kikomo za ndani kila mwezi ili kulinda maslahi ya watumiaji na kuhakikisha ushindani wa haki katika soko la mafuta nchini.

EWURA imeeleza kuwa,bei za mafuta katika mwezi Mei 2026 zimeathiriwa na mivutano ya kisiasa na kijeshi katika ukanda wa Mashariki ya Kati, hususan kuhusisha nchi za Marekani, Israeli na Iran.

Migogoro hiyo imesababisha mashambulizi katika miundombinu ya uzalishaji, uhifadhi na usafirishaji wa mafuta, hali iliyopunguza upatikanaji wa bidhaa hizo katika soko la dunia.

Aidha, kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz ambayo ni njia muhimu inayopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta ya dunia kumeongeza changamoto katika usambazaji, kusababisha kupanda kwa gharama za usafirishaji na bima za meli.

Matokeo yake ni msongamano wa meli, ucheleweshaji wa mizigo na hatimaye kupanda kwa bei za mafuta kimataifa.

Kutokana na utegemezi mkubwa wa Tanzania kwa mafuta kutoka Mashariki ya Kati, athari za mabadiliko hayo zimeonekana moja kwa moja katika soko la ndani.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa ruzuku ya takribani shilingi 259 kwa kila lita moja ya dizeli ili kupunguza athari za ongezeko la bei kwa wananchi na sekta muhimu za uchumi.

Dizeli ni nyenzo muhimu katika shughuli za uzalishaji viwandani, usafirishaji wa bidhaa na huduma za kijamii.

Kwa mwezi Mei 2026, bei kikomo za rejareja katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ni kama ifuatavyo:

Dar es Salaam:

Petroli shilingi 4,115; Dizeli shilingi 4,248; Mafuta ya taa shilingi 4,677.

Tanga:

Petroli shilingi 4,176; Dizeli shilingi 4,309; Mafuta ya taa shilingi 4,738.

Mtwara:

Petroli shilingi 4,207; Dizeli shilingi 4,341; Mafuta ya taa shilingi 4,770.

Bei za jumla pia zimebadilika, ambapo kwa Dar es Salaam petroli ni shilingi 3,972.13, dizeli shilingi 4,104.81 na mafuta ya taa shilingi 4,533.34 kwa lita.

EWURA imebainisha kuwa bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) ziliongezeka kwa viwango vikubwa mwezi Aprili 2026.

Kwa mfano, petroli, dizeli na mafuta ya taa zilifikia wastani wa dola za Marekani 71.76, 85.99 na 85.34 kwa pipa mtawalia, zikionesha ongezeko la kati ya asilimia 71 hadi 122 ikilinganishwa na vipindi vya nyuma.

Aidha, gharama za uagizaji wa mafuta kupitia Bandari ya Dar es Salaam ziliongezeka kwa wastani wa asilimia 6.2 kwa petroli, asilimia 5.4 kwa dizeli na asilimia 7.2 kwa mafuta ya taa.

Kwa upande wa ubadilishaji wa fedha za kigeni, EWURA imeeleza kuwa,wastani wa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani uliimarika kwa takribani asilimia 3.7, hatua iliyosaidia kwa kiasi fulani kupunguza makali ya ongezeko la bei.

EWURA imewataka wafanyabiashara wa mafuta kuuza bidhaa zao kwa kuzingatia bei kikomo zilizotangazwa, huku ikionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka maelekezo hayo.

Pia vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuonyesha bei kwenye mabango yanayoonekana wazi kwa wateja, na kutoa stakabadhi halali za mauzo kupitia mifumo ya kielektroniki (EFPP). Wananchi wamehimizwa kudai risiti na kuripoti ukiukwaji wowote wa bei.

Kwa ujumla, mabadiliko ya bei za mafuta mwezi Mei 2026 yanaakisi hali halisi ya soko la dunia lililoathiriwa na migogoro ya kisiasa na changamoto za usambazaji.

Serikali, kupitia EWURA, inaendelea kusimamia soko na kuchukua hatua za kupunguza athari kwa wananchi huku ikihimiza uwazi na ushindani wa haki katika biashara ya mafuta nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here