MOROGORO-Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Kiislamu ya Bohora Duniani (Da'i al-Mutlaq), Syedna Mufaddal Saifuddin Saheb, (mwenye picha yake pekee) mapema leo Mei 16, 2026, amesafiri kwa treni ya SGR kati ya Dar es salaam na Morogoro akiambatana na viongozi na waumini zaidi ya 70 wa dhehebu hilo nchini, kutembelea waumini wake mkoani Morogoro.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu,Mhandisi Machibya Shiwa.
Syedna Mufaddal Saifuddin ni kiongozi wa 53 wa kiroho wa dhehebu hili lenye wafuasi zaidi ya milioni 1 duniani kote. Jamii hii inajulikana kwa misingi thabiti ya utendaji kazi, biashara, uwekezaji, mshikamano wa kijamii, na utunzaji wa mazingira nk.
Kiongozi huyu wa madhehebu ya Kiislamu ya Bohora Duniani, kusafiri na SGR, tafsiri zake ni hizi:
Kuonyesha imani kwa usalama na ubora wa SGR
Kiongozi huyo ni miongoni mwa viongozi wa kidini wenye heshima kubwa duniani. Kuchagua kusafiri kwa SGR ni ishara ya kuamini usalama, ubora, utulivu na hadhi ya huduma ya reli ya kisasa nchini Tanzania.
Diplomasia ya Usafiri
Safari yake pamoja na viongozi na waumini zaidi ya 70 wa Bohora ni aina ya “diplomasia ya usafiri”, ambapo wageni wa kimataifa wanakuwa mabalozi wa kuitangaza SGR kwa dunia kupitia uzoefu wao binafsi.
Kuongeza hadhi ya Tanzania kama kitovu cha miundombinu ya kisasa Afrika Mashariki
Kutumika kwa SGR na viongozi wa kimataifa, kunaonyesha kuwa Tanzania imefikia kiwango cha miundombinu kinachoweza kuaminiwa na watu wa hadhi mbalimbali duniani.
Ujio wa viongozi na waumini wengi Morogoro kupitia SGR, kunasaidia kuongeza shughuli za kiuchumi kama hoteli, usafiri wa ndani, chakula na biashara ndogondogo.
Uthibitisho kuwa SGR si mradi wa kawaida bali chachu ya maendeleo
SGR sasa inaonekana si tu njia ya usafiri, bali sehemu ya kuunganisha jamii, dini, biashara na diplomasia ya Tanzania.
Kuimarisha taswira ya TRC na huduma za reli
Kitendo cha viongozi wakubwa wa dini kutumia reli kinajenga imani zaidi kwa wananchi kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa na Tanzania Railways Corporation kupitia treni za SGR.



.jpg)