Kocha Gamondi atangaza kikosi cha Taifa Stars

NA DIRAMAKINI

KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars),Miguel Gamondi ametangaza kikosi cha wachezaji wa timu ya taifa kitakachoingia kambini kujiandaa na michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa iliyopo kwenye kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) dhidi ya Uganda na Rwanda.
Gamondi ameendelea kuwapa nafasi wachezaji wanaofanya vizuri ndani na nje ya nchi huku akilenga kujenga timu imara yenye ushindani kuelekea michuano na mashindano ya kimataifa yajayo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF, kambi hiyo inalenga kuimarisha kiwango cha timu pamoja na kuwapa nafasi benchi la ufundi kutathmini uwezo wa wachezaji katika mfumo mpya wa kiuchezaji unaotarajiwa kutumiwa katika mechi zijazo za ushindani.

Katika kikosi hicho, makipa walioitwa ni Zuber Foba wa Azam FC, Aishi Manula wa Azam FC pamoja na Yona Amos wa Pamba Jiji FC.

Safu ya mabeki inaundwa na Pascal Msindo wa Azam FC, Nickson Kibabage wa Simba SC, Ibrahim Hamad na Bakari Mwamnyeto wa Young Africans SC, Elias Lawi wa Azam FC, Vedastus Masinde wa Simba SC pamoja na Mohamed Mussa wa Mashujaa FC.

Upande wa kiungo, kocha Gamondi amewajumuisha Haji Mnoga anayekipiga katika klabu ya Salford City, Novatus Dismas wa Göztepe SK, Mohammed Sagaf wa Eastbourne Borough FC, Abdulkarim Kiswanya wa Namungo FC, Mudathiri Yahya wa Young Africans SC, Charles M’mombwa wa Floriana FC, Alphonce Mabula wa Shamakhi FK, Bakari Msimu wa Coastal Union FC pamoja na Tarryn Allarakhia wa Rochdale AFC.

Katika safu ya ushambuliaji, Taifa Stars itawategemea Feisal Salum wa Azam FC, Simon Msuva wa Al-Talaba SC, Selemani Mwalimu wa Simba SC, Cyprian Kachwele wa HFX Wanderers FC pamoja na Said Khamis anayekipiga nchini Malaysia.

Ujumuishaji wa wachezaji wanaocheza nje ya Tanzania unaonyesha dhamira ya benchi la ufundi kuongeza ushindani ndani ya kikosi hicho huku likichanganya uzoefu wa kimataifa na vipaji vya ndani vinavyoendelea kung’ara katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Aidha, michezo hiyo ya kirafiki dhidi ya Uganda na Rwanda inatarajiwa kuwa kipimo muhimu kwa Taifa Stars katika kujiandaa na majukumu ya baadaye ikiwemo mechi za kufuzu mashindano ya kimataifa.

Benchi la ufundi linatarajiwa kutumia michezo hiyo kuangalia muunganiko wa kikosi, uimara wa safu ya ulinzi pamoja na makali ya ushambuliaji.

Mashabiki wa soka nchini wamepokea kwa hamasa kubwa tangazo hilo la kikosi, huku wengi wakielekeza matumaini yao kwa wachezaji wenye uzoefu pamoja na chipukizi waliopata nafasi ya kuitumikia taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here