MSD ilivyoandika historia mpya katika kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini

NA GODFREY NNKO

UPATIKANAJI wa bidhaa za afya kama vile dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara ni msingi muhimu katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
Katika kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa gharama nafuu, Bohari ya Dawa (MSD) imeendelea kuwa mhimili mkuu wa mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini Tanzania.

Miaka ya hivi karibuni, taasisi hiyo imepiga hatua kubwa katika kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya vya umma, hatua inayotajwa kuchochea mageuzi makubwa ya sekta ya afya nchini.

Mafanikio hayo yamebainishwa Aprili 24, 2026, wakati wa semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika katika Ofisi za MSD Kanda ya Kati, Kizota mkoani Dodoma, ambapo viongozi wa taasisi hiyo walieleza namna juhudi mbalimbali zilivyochangia kuimarika kwa huduma za afya nchini.
Akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Mavere Tukai amesema, taasisi hiyo ina jukumu la msingi la kuhakikisha bidhaa zote za afya zinapatikana kwa uhakika nchini, kwa kuwa bila bidhaa hizo mfumo wa huduma za afya hauwezi kuwa kamili.

Bw.Tukai amesema,MSD inasimamia upatikanaji wa bidhaa za afya zilizo bora, salama kwa matumizi ya wananchi, zenye gharama nafuu na zinazowafikia walengwa kwa wakati.

Kupitia mfumo wa utoaji huduma za afya nchini, amesema vituo vya kutolea huduma humgusa mwananchi moja kwa moja huku MSD ikiwa kiungo muhimu kinachohakikisha bidhaa muhimu za afya zinapatikana muda wote.
"Tuna majukumu makubwa manne ya kuzalisha, kununua, kuhifadhi bidhaa za afya katika maghala pamoja na kusambaza bidhaa hizo kwa wateja,”amesema Bw. Tukai.

Ameongeza kuwa, MSD kwa sasa ndiyo msambazaji mkuu wa bidhaa za afya katika vituo vya umma kwa wastani wa asilimia 81 hadi 83, huku asilimia iliyobaki ikikamilishwa na washirika wengine katika ngazi za mikoa.

Utimilifu wa bidhaa waongezeka maradufu

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, MSD imefanikiwa kuongeza kiwango cha utimilifu wa bidhaa za afya kutoka asilimia 40 hadi kufikia asilimia 80, hatua inayotafsiriwa kama mafanikio makubwa katika kuimarisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini.

Kwa mujibu wa Bw. Tukai, mafanikio hayo yametokana na maboresho ya mifumo ya kiutendaji pamoja na juhudi za Serikali kuhakikisha fedha za kutosha zinapatikana kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya.
Aidha, upatikanaji wa bidhaa za afya ashiria umeongezeka kutoka asilimia 42 mwaka 2021/22 hadi asilimia 73 kufikia Machi 2026. Hii inahusisha bidhaa 382 za msingi pamoja na bidhaa 73 za miradi maalum.

Ongezeko hilo lina maana kuwa,vituo vingi vya afya sasa vina uwezo wa kuwa na akiba ya kutosha ya dawa na vifaa tiba kwa kipindi kisichopungua mwezi mmoja, hali inayopunguza uhaba uliokuwa ukijitokeza mara kwa mara hapo awali.

Mapato yaongezeka kwa zaidi ya asilimia 100

Kwa upande wa kifedha, MSD imeonesha ukuaji mkubwa ambapo mapato yameongezeka kwa asilimia 103 kutoka Shilingi bilioni 315.12 hadi kufikia Shilingi bilioni 640.5 mwaka 2024/25.

Ukuaji huo unaashiria kuimarika kwa shughuli za taasisi pamoja na kuongezeka kwa uwezo wake wa kuhudumia mahitaji ya vituo vya afya nchini.
Sambamba na hilo, taasisi hiyo imeongeza mizunguko ya usambazaji wa bidhaa kutoka mara nne hadi sita kwa mwaka, hatua iliyosaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma.

Ujenzi wa Maghala na uwekezaji wa kimkakati

Aidha,katika kuimarisha mfumo wa uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya, MSD imewekeza katika ujenzi wa maghala ya kisasa yanayokidhi viwango vya kimataifa vya uhifadhi wa bidhaa hizo.

Maghala hayo yamejengwa katika kanda za Dodoma na Mtwara, kila moja likiwa na ukubwa wa mita za mraba 12,000, huku ujenzi wa ghala jingine ukiendelea katika eneo la Chato mkoani Geita.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa kuhifadhi bidhaa za afya na kuhakikisha usambazaji unakuwa wa haraka na wenye ufanisi zaidi.

Uzalishaji wa ndani wapewa kipaumbele

Pia,katika jitihada za kupunguza utegemezi wa bidhaa za afya kutoka nje ya nchi, MSD imeanzisha kampuni tanzu ya Medipharm Manufacturing Company pamoja na kukamilisha kiwanda cha kutengeneza mipira ya mikono katika eneo la Idofi.
Hatua hiyo imeenda sambamba na ongezeko kubwa la ununuzi wa bidhaa kutoka kwa wazalishaji wa ndani, ambapo thamani ya manunuzi hayo imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 15.90 hadi Shilingi bilioni 98.72 ndani ya kipindi cha miaka minne.

Wachambuzi wa sekta ya afya wanaeleza kuwa, uwekezaji huo utaongeza uhakika wa upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya na kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani.

Gharama za Dialysis zapungua

MSD pia imeendelea kuunga mkono huduma za kibingwa nchini, hususan matibabu ya figo. Kupitia usambazaji wa mashine 162 za dialysis katika hospitali mbalimbali nchini, gharama za matibabu kwa mgonjwa mmoja zimepungua kutoka wastani wa Shilingi 179,000 hadi Shilingi 70,160.

Hatua hiyo imeongeza upatikanaji wa huduma za dialysis kwa wananchi wengi zaidi, hasa wale waliokuwa wakishindwa kumudu gharama kubwa za matibabu hayo hapo awali.

Changamoto ya madeni bado ni kikwazo

Pamoja na mafanikio hayo, MSD bado inakabiliwa na changamoto ya madeni kutoka katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo, hadi Desemba 2025 deni lilikuwa limefikia Shilingi bilioni 141, japokuwa lilionyesha punguzo la asilimia saba ikilinganishwa na mwezi Juni wa mwaka huo.

Madeni hayo yanaelezwa kuathiri utekelezaji wa majukumu ya MSD kwa kuchelewesha malipo kwa wazabuni, kuongeza gharama za ununuzi na wakati mwingine kusababisha ucheleweshaji wa usambazaji wa bidhaa.

Aidha, hali hiyo hupunguza uwezo wa taasisi kuchukua hatua stahiki dhidi ya wazabuni wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati.

Mahitaji yaongezeka kadri vituo vinavyoongezeka

Katika kipindi cha miaka tisa iliyopita, idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya nchini imeongezeka kutoka 5,642 mwaka 2016/17 hadi zaidi ya 8,893 mwaka 2025.

Ongezeko hilo limeongeza kwa kiwango kikubwa mahitaji ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara, hivyo kuongeza shinikizo katika mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya.

Kutokana na hali hiyo, MSD inalazimika kuendelea kuwekeza zaidi katika miundombinu, mifumo ya kidijitali na uwezo wa kuhifadhi bidhaa ili kuendana na kasi ya mahitaji.

Mfumo wa kisasa wa kudhibiti gharama

Vilevile, katika kuimarisha uwazi na ufanisi wa matumizi ya rasilimali, MSD imeanza kutumia mfumo wa kisasa wa Time-Driven Activity-Based Costing (TDABC).
Mfumo huo unalenga kuboresha usimamizi wa gharama kwa kubainisha matumizi halisi ya rasilimali katika mnyororo wa ugavi, hatua inayotarajiwa kuongeza tija na uwajibikaji katika utoaji wa huduma.

Afya ni Usalama wa Taifa

Akizungumzia umuhimu wa sekta ya afya, Bw. Tukai amesema afya ya jamii ina uhusiano wa moja kwa moja na maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa.

“Afya ni usalama wa taifa.Jamii ikiwa haina afya haiwezi kuwa salama, na bila usalama hakuna uzalishaji, hivyo hakuna uchumi,” amesema.

Amefananisha sekta ya afya na stuli ya miguu mitatu inayojumuisha fedha, huduma na bidhaa, huku MSD ikiwa na jukumu la kuhakikisha bidhaa za afya zinapatikana muda wote.

Kwa mujibu wake, kuyumba kwa nguzo moja kunaweza kuathiri mfumo mzima wa utoaji huduma za afya.

Serikali yapongeza

Kwa upande wake, mwakilishi wa Wizara ya Afya, Mfamasia Bi. Anneth Wilbroad amesema, wizara hiyo inathamini mchango wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya na kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi.

Naye mwakilishi wa Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Bi. Magreth Makilika ameipongeza MSD kwa kuendeleza ushirikiano na vyombo vya habari, akisema hatua hiyo ni mfano mzuri wa uwazi na uwajibikaji katika taasisi za umma.
Kwa upande mwingine, mwakilishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kutoka Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Bw. Hassan kwa niaba ya Dkt.Rashid Mfaume amesema,wanahabari wana nafasi muhimu katika kuunganisha jamii na taasisi za Serikali pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya maendeleo.

Wahariri waipongeza MSD

Akizungumza kwa niaba ya wahariri, Mhariri Mkuu wa Gazeti la Habarileo, Bw. Mgaya Kingoba amesema,semina hiyo imechangia kuongeza uelewa sahihi kuhusu sekta ya afya na kusaidia kupunguza upotoshaji wa taarifa.

Amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa sahihi na zenye kuaminika kuhusu uwekezaji wa Serikali katika sekta ya afya.

“Nafasi yetu ni kuwa daraja kati ya Serikali na wananchi kwa kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia walengwa. Hili linahitaji weledi na uwajibikaji wa hali ya juu,” amesema.

Wahariri wajionea mafanikio

Katika hatua nyingine, wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari walitembelea Hospitali ya Jiji Dodoma pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, ambako walijionea maboresho makubwa ya huduma za afya yaliyotokana na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kupitia MSD.

Wakiwa katika Hospitali ya Jiji Dodoma, Mganga Mfawidhi Dkt. Joshua Mwalongo amesema, hospitali hiyo imefanikiwa kutoa huduma mbalimbali za kibingwa kutokana na uwekezaji wa Serikali na ushirikiano wa karibu na MSD.

Amesema,upatikanaji wa dawa muhimu umefikia zaidi ya asilimia 92, hali iliyopunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya wagonjwa kukosa huduma.

Mfamasia wa hospitali hiyo, Bi. Margret Mhalule amesema,ongezeko la bajeti ya dawa limeiwezesha MSD kusambaza bidhaa kwa wakati na hivyo kupunguza malalamiko ya wananchi.

Kwa upande wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt. Bwire Robert amesema,matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kuagiza dawa yameongeza kasi ya upatikanaji wa huduma na kupunguza ucheleweshaji.

Moja ya mafanikio makubwa yaliyojitokeza Manyoni ni kuanzishwa kwa huduma maalum za watoto wachanga njiti kupitia vifaa vya kisasa vilivyopatikana kwa msaada wa MSD.

Kwa mujibu wa Dkt. Bwire, uwekezaji huo umechangia kupunguza vifo vya watoto njiti kwa zaidi ya asilimia 90.

Ufanisi waongezeka

Awali, Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma, Bi. Mwanashehe Jumaa amesema,kanda hiyo kwa sasa inahudumia zaidi ya vituo 840 vya afya katika mikoa ya Dodoma, Singida pamoja na Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.

Amesema,mfumo wa ugawaji wa huduma umeboreshwa kwa kuyagawa maeneo hayo katika makundi mawili ili kuongeza ufanisi wa usambazaji wa dawa na vifaa tiba.

Kwa mujibu wake, kila kundi hupatiwa huduma mara sita kwa mwaka kwa mzunguko wa kila baada ya miezi miwili.

“Kwa mfano, iwapo mwezi Aprili tunahudumia Mkoa wa Dodoma, basi mwezi Mei tunahudumia Mkoa wa Singida. Mfumo huu umetusaidia kufikia vituo vyote kwa ufanisi na kwa wakati,”amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa MSD ipo tayari kukabiliana na hali za dharura zikiwemo milipuko ya magonjwa au mahitaji ya ghafla ya vifaa tiba.

Mwanzo wa enzi mpya

Kwa ujumla, mafanikio ya MSD yanaendelea kuonesha mwelekeo mpya wa sekta ya afya nchini, ambapo wananchi wanaanza kupata huduma bora, za uhakika na kwa wakati.

Hata hivyo, wataalamu wanaeleza kuwa ili mafanikio hayo yawe endelevu, kuna haja ya kuongeza uwekezaji katika uzalishaji wa ndani na kuboresha zaidi mifumo ya ugavi ikiwemo madeni kulipwa kwa wakati.

Hatua hizo zitasaidia kuhakikisha kuwa, huduma bora za afya zinawafikia wananchi wote kwa usawa,ufanisi na wakati unaotakiwa katika vituo mbalimbali vya afya nchini.
MSD ni taasisi iliyoundwa kisheria mwaka 1993 ikifuatiwa na maboresho mbalimbali ya sheria ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake ya msingi ambapo dira yake ni kuwa kituo cha ubora kwa mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya barani Afrika.

Aidha,dhamira ya MSD ni kutoa huduma bora na za uhakika kwa vituo vya kutolea huduma
za afya ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here