NA DIRAMAKINI
RAIS wa Marekani, Donald J. Trump, ametangaza kuondoa ushuru na vikwazo vilivyokuwa vinaathiri biashara ya mvinyo (pombe) aina ya whisky na bourbon kati ya Scotland na jimbo la Kentucky nchini humo.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ziara ya heshima ya Mfalme na Malkia wa Uingereza nchini Marekani, waliotembelea Ikulu ya White House kabla ya kurejea nchini kwao.
Katika taarifa yake, Rais Trump ameeleza kuwa, uamuzi huo unalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Scotland na Kentucky, maeneo mawili yanayotambulika kimataifa kwa uzalishaji wa vinywaji hivi muhimu.
Amebainisha kuwa, sekta ya whisky nchini Scotland na ile ya bourbon huko Kentucky ni mihimili mikubwa ya uchumi katika maeneo hayo, hivyo kuondolewa kwa vikwazo kutachochea ukuaji wa biashara na ajira.
Kwa muda mrefu, wadau wa sekta hizo walikuwa wakitaka kuondolewa kwa vizuizi hivyo, wakisisitiza umuhimu wa biashara ya kimataifa, hususan katika usambazaji wa mapipa ya mbao yanayotumika kuhifadhia na kukomaza vinywaji hivyo.
Ushirikiano huo wa kihistoria umechangia kwa kiasi kikubwa ubora na sifa ya bidhaa hizo katika soko la dunia.
Rais Trump pia alieleza kuwa hatua hiyo imechangiwa na mazungumzo na viongozi wa kifalme wa Uingereza, akisisitiza kuwa walifanikiwa kushawishi mabadiliko hayo kwa njia ya kipekee.
Aidha, alieleza kuwa ni heshima kubwa kwa Marekani kuwapokea viongozi hao wa kifalme.
Uamuzi huu unatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kibiashara kati ya Marekani na Uingereza, huku ukitoa fursa kwa wazalishaji na wafanyabiashara kunufaika na mazingira bora ya soko huria.
