NA DIRAMAKINI
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema wizara yake imeanza kupitia taratibu za kisheria na kiutawala zitakazoweza kumwezesha nyota wa klabu ya Simba SC, Clatous Chama kupata uraia wa Tanzania kufuatia kiwango chake bora alichokionyesha katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans SC.
Kauli hiyo ilitolewa Mei 9, 2026 wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za wanamichezo bora wa mwaka iliyoandaliwa na National Sports Council (NSC) katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo iliwakutanisha viongozi wa michezo, wanamichezo, wadau wa sekta ya michezo pamoja na mashabiki mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya nchi.
Akizungumza mbele ya wageni waalikwa na wadau wa michezo, Makonda alisema bao la kipekee lililofungwa na Chama katika mchezo uliochezwa Mei 3, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo limeonyesha kiwango cha juu cha ubora na mchango mkubwa wa mchezaji huyo katika maendeleo ya soka la Tanzania.
“Kwa lile goli zuri la Chama, wizara imeanza mchakato wa kuona taratibu za kumpatia uraia kwa lengo la kuongeza tija na nguvu katika timu yetu ya taifa. Chama ameonyesha uwezo mkubwa na ameweza kubadilika kulingana na wakati na mahitaji ya mchezo,” alisema Makonda.
Kauli hiyo imeibua mjadala mpana miongoni mwa wadau wa michezo nchini, huku baadhi wakieleza kuwa hatua hiyo inaonyesha namna Serikali inavyothamini mchango wa wachezaji wa kigeni wanaoshiriki ligi ya Tanzania na kusaidia kuinua kiwango cha ushindani wa soka nchini.
Clatous Chama ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni waliopata mafanikio makubwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, akiwa ameisaidia Simba SC kutwaa mataji mbalimbali ya ndani pamoja na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa barani Afrika. Umahiri wake wa kucheza eneo la kiungo mshambuliaji umeendelea kumfanya kuwa tegemeo muhimu ndani ya kikosi hicho.
Hata hivyo, pamoja na kauli ya Waziri Makonda kuhusu uraia, taratibu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu duniani, FIFA, zinaeleza kuwa mchezaji ambaye tayari ameichezea timu ya taifa ya nchi moja katika mashindano rasmi hawezi kuichezea timu ya taifa ya nchi nyingine isipokuwa katika mazingira maalumu yanayoruhusiwa kikanuni.
Kwa sasa, Chama tayari ni mchezaji wa timu ya taifa ya Zambia, hali inayomaanisha kuwa hata kama angepata uraia wa Tanzania, bado asingekuwa na sifa za kuichezea Taifa Stars kwa mujibu wa kanuni za FIFA.
Wadau wa michezo wameendelea kutoa maoni tofauti kuhusu suala hilo, huku wengine wakisisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika ukuzaji wa vipaji vya wazawa ili kuijengea nguvu ya kudumu timu ya taifa, badala ya kutegemea mchakato wa kuwapa uraia wachezaji wa kigeni.
Kauli ya Makonda imekuja katika kipindi ambacho ushindani wa soka la Tanzania unaendelea kukua kwa kasi, huku vilabu vikubwa vya nchini vikiongeza uwekezaji katika usajili wa wachezaji wenye uwezo mkubwa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
