Serikali yakamilisha Mfumo wa Kidijiti wa Mashindano ya Walimu Mahiri,walimu 2,800 wawasilisha video za ufundishaji

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema, imekamilisha ujenzi wa mfumo wa kidijiti wa mashindano ya walimu wa stadi za kufundishia utakaotumiwa na walimu wa shule za msingi na sekondari katika masomo yote nchini, hatua inayolenga kuongeza ubora wa ufundishaji na kuibua walimu mahiri.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Mei 7,2026 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa, hadi sasa jumla ya walimu 2,800 wamewasilisha video zao za ufundishaji kupitia mfumo huo kwa ajili ya tathmini.

Profesa Mkenda amesema,mfumo huo umeongeza ufanisi katika mchakato wa kuwatambua walimu wenye ubunifu na umahiri mkubwa wa kufundisha, ambao watapatiwa zawadi mbalimbali pamoja na fursa ya kurekodi video za mfano zitakazotumiwa na walimu wengine katika shughuli za ufundishaji na ujifunzaji.

Ameeleza kuwa, matumizi ya teknolojia katika tathmini ya walimu ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha sekta ya elimu kwa kuhimiza matumizi ya mbinu za kisasa za ufundishaji na kuongeza ubora wa elimu nchini.
Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda amesema,Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa vifaa vya kielimu na saidizi kwa walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuhakikisha usawa na ujumuishi katika elimu.

Amesema,Serikali imenunua na kusambaza vifaa mbalimbali kwa walimu, wakufunzi na walimu tarajali wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kompyuta mpakato 688, mashine za kidijiti za kurekodi sauti 377, tablet 196, mashine za Breili za kieletroniki 19, emboza sita, mashine saba za kuongeza sauti pamoja na seti nne za kupima usikivu.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, vifaa hivyo vimesambazwa katika shule za msingi 309, shule za sekondari 629 pamoja na vyuo vya ualimu nchini kote.
Aidha, amesema wanufaika wa vifaa hivyo ni pamoja na watu wenye ulemavu wa viungo 342, wenye changamoto ya uoni 312, wenye uziwi 155, wenye ualbino 190 na wenye usikivu hafifu 198.

Profesa Mkenda amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu jumuishi ili kuhakikisha kila mwanafunzi na mwalimu anapata mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia bila kujali changamoto walizonazo.

Kuhusu maendeleo ya mafunzo kwa walimu, Waziri Mkenda amesema, mafunzo endelevu ni nyenzo muhimu katika kuimarisha utendaji kazi wa walimu, wakufunzi, wathibiti ubora wa shule pamoja na wasimamizi wa elimu nchini.

Amesema, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa walimu na wanafunzi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mtaala na matumizi ya teknolojia kwenye elimu.

Pia katika kipindi hicho, amesema Serikali imetoa mafunzo kwa walimu na wanafunzi 206,296 kuhusu matumizi ya majukwaa ya kidijiti na maktaba mtandao, hatua inayolenga kuwawezesha kutumia nyenzo za kidijiti katika ufundishaji na ujifunzaji.

Vilevile, walimu 124,601 wamepatiwa mafunzo mbalimbali ikiwemo kuhusu ufundishaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ambapo walimu 34,305 walishiriki, huku wakuu wa shule 379 wakipata mafunzo ya usimamizi na utekelezaji wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini.
Aidha, walimu 89,917 wa shule za msingi na sekondari wamepatiwa mafunzo kuhusu mbinu mbalimbali za kuboresha ufundishaji na ujifunzaji darasani.

Profesa Mkenda amesema, hatua hizo zinaimarisha umahiri wa walimu, kuongeza ubora wa ujifunzaji darasani na kuweka msingi imara wa mafanikio ya mageuzi ya elimu nchini.

Ameongeza kuwa,Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha mfumo wa elimu unazalisha wahitimu wenye ujuzi na maarifa yanayokidhi mahitaji ya taifa la sasa na la baadaye.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here