Rais Samia anaendelea kupeleka furaha na neema kwa watumishi wa umma Tanzania-Waziri Ridhiwani Kikwete

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza mageuzi makubwa yanayolenga kuboresha maslahi, ustawi na mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma nchini.
Akizungumza katika mkutano wa maafisa tawala na maafisa rasilimaliwatu uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha,Waziri Kikwete amesema watumishi wa umma wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi,uadilifu na kujituma ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ubora unaostahili.

Amesema,dhamira ya Serikali ni kuhakikisha watumishi wa umma wanapata mazingira bora ya kazi yanayowawezesha kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa zaidi, huku akisisitiza kuwa ustawi wa watumishi hao una mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Pia, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amewakumbusha umuhimu wa kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya utumishi wa umma, ili nao waweze kuleta furaha na neema kwa Watanzania kupitia huduma bora wanazozitoa.

Aidha, Waziri huyo ameeleza kuwa,Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kihistoria katika kuboresha maslahi ya watumishi wa umma, hatua ambazo zinaakisi dhamira ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya utumishi wa umma nchini.

Miongoni mwa hatua hizo ni uamuzi wa Serikali kupandisha madaraja watumishi wa umma 219,042 nchini, hatua iliyotajwa kuwa ni moja ya maboresho makubwa katika historia ya utumishi wa umma Tanzania.

Sambamba na hilo, Serikali imeongeza mishahara ya watumishi wa umma kwa asilimia zaidi ya 35.1 mwaka 2025, huku kiwango cha chini cha mishahara katika sekta binafsi kikiongezwa kwa asilimia zaidi ya 33.4 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Maboresho hayo yanatarajiwa kuleta tija kubwa katika sekta mbalimbali za uchumi na huduma za jamii ikiwemo afya, elimu, kilimo, mawasiliano, usafirishaji, nishati, viwanda, biashara, hoteli, michezo, uvuvi, sekta ya bahari, madini pamoja na utamaduni.

Kwa mujibu wa Waziri Kikwete, takwimu hizo zinaonesha wazi kasi ya mageuzi ya kiutumishi yanayoendelea kutekelezwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, ambayo imeweka mkazo katika ustawi wa watumishi wa umma, ufanisi wa taasisi za Serikali na maendeleo endelevu ya taifa.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na watumishi wa umma katika kujenga mfumo imara wa kiutumishi unaozingatia uwajibikaji, haki na usawa, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazokidhi mahitaji yao na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here