Serikali yarejesha wanafunzi 3,467 shuleni, yaimarisha fursa za elimu ya juu na teknolojia ya akili unde

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imefanikiwa kuwarejesha shuleni wanafunzi 3,467 waliokuwa wamekatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali, ambapo wanawake ni 2,062 na wanaume 1,405. Wanafunzi hao wanaendelea na masomo kupitia mfumo wa elimu kwa njia mbadala.
Hayo yameelezwa leo Mei 7, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Profesa Mkenda amesema,Serikali pia imefanya tathmini ya utekelezaji wa sera na miongozo ya kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali.

Amesema,tathmini hiyo imebaini mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazoweza kuathiri utekelezaji wa sera hizo.

Katika hatua nyingine, Serikali imeendelea kupanua fursa za elimu ya juu nchini kupitia utoaji wa mikopo na uratibu wa udahili wa wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu.

Waziri Mkenda amesema, kwa mwaka wa masomo 2025/2026, Serikali iliratibu udahili wa wanafunzi 170,916 walioomba kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza katika vyuo vya elimu ya juu nchini.

Kati ya waombaji hao, wanafunzi 159,010 sawa na asilimia 93 walidahiliwa ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 21,193 ikilinganishwa na wanafunzi 137,817 waliodahiliwa mwaka wa masomo 2024/2025.

Aidha, Serikali imetoa mikopo kwa wanafunzi 287,120 wa elimu ya juu katika mwaka wa masomo 2025/2026 ikilinganishwa na wanafunzi 245,384 waliopata mikopo mwaka uliopita.

Kati ya wanufaika hao, wanafunzi wa mwaka wa kwanza ni 106,606 huku wanaoendelea na masomo wakiwa 177,881.

Akizungumzia maendeleo ya teknolojia duniani, Profesa Mkenda amesema,Serikali imeanza kuchukua hatua mahsusi za kujenga uwezo wa taifa katika matumizi na usimamizi wa teknolojia ya Akili Unde (AI), akisema teknolojia hiyo ni fursa kubwa kwa maendeleo ya sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, elimu,ulinzi na usalama.

Amesema,pamoja na manufaa yake, teknolojia ya akili unde inaweza pia kuleta changamoto kubwa iwapo nchi haitakuwa na uwezo wa kuielewa,kuimudu na kuisimamia ipasavyo.

“Akili unde inaweza kubadilisha kwa kiwango kikubwa muundo wa ajira duniani na kusababisha watu wengi kupoteza ajira kutokana na maendeleo ya haraka ya teknolojia. Pia inaweza kuathiri masuala ya ulinzi, usalama na faragha ya taarifa za watu,” amesema Profesa Mkenda.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imeanzisha mpango maalumu wa kufadhili vijana wa Kitanzania kusomea masuala ya akili unde na teknolojia za kisasa kupitia mpango unaojulikana kama Samia Scholarship Extended DS/AI+.

Kwa mujibu wa Waziri Mkenda, wanafunzi 50 waliofanya vizuri zaidi katika tahasusi za sayansi zenye masomo ya hisabati kwenye mtihani wa kidato cha sita mwaka 2025 walichaguliwa kwa ushindani na uwazi ili kunufaika na mpango huo.

Amesema,wanafunzi hao walipewa mafunzo maalumu ya maandalizi katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyopo Arusha kabla ya kuanza masomo yao nje ya nchi.

“Kati ya wanafunzi hao 50, wanafunzi 16 tayari wameanza masomo katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini, huku wanafunzi 34 waliobaki wakikubaliwa kujiunga na vyuo vikuu nchini Ireland,”amesema.

Amefafanua kuwa, wanafunzi 32 watajiunga na Chuo Kikuu cha Limerick huku wawili wakijiunga na Chuo Kikuu Kishiriki cha Dublin nchini Ireland, na wanatarajiwa kuondoka nchini mwezi Septemba mwaka huu.

Profesa Mkenda amesema,wanufaika wa mpango huo wamepata punguzo la ada kwa asilimia 50 katika Chuo Kikuu cha Limerick kufuatia makubaliano yaliyosainiwa Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam.

Amesema, makubaliano hayo yamelenga kuongeza fursa za elimu ya juu kwa vijana wa Kitanzania katika fani za kisasa kama Sayansi Data, Akili-Unde na Sayansi Shirikishi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza rasilimali watu wenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta ya teknolojia.

Kwa upande wa wanafunzi 16 waliokwenda Chuo Kikuu cha Johannesburg, Waziri huyo amesema, wamefaidika na utaratibu wa ushirikiano wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaowaruhusu wanafunzi kutoka nchi wanachama kulipa ada nafuu ikilinganishwa na wanafunzi kutoka mataifa mengine.

Ameongeza kuwa,mpango huo ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, inayosisitiza umuhimu wa kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi katika maeneo ya sayansi,teknolojia,uhandisi na hisabati.

Waziri Mkenda ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wadau wa elimu nchini kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia Mfuko wa Samia Scholarship ili kuongeza idadi ya wataalamu wa sayansi na teknolojia nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here