Sheria mpya za uhamiaji Japan zageuka kilio, adai ameishi miaka 30 hawezi kurudi India na watoto wake wanazungumza Kijapani pekee

NA DIRAMAKINI

RAIA wa India anayefanya biashara ya mgahawa nchini Japan, Manish Kumar ameibua mjadala mkubwa kuhusu sera mpya za uhamiaji baada ya kuangua kilio hadharani akielezea hofu ya kufukuzwa nchini humo alikoishi kwa takribani miaka 30 pamoja na familia yake.
Kumar ambaye anamiliki mgahawa wa vyakula vya Kihindi katika jimbo la Saitama karibu na mji wa Tokyo, amesema maisha yake yote pamoja na familia yake yamejengwa nchini Japan kiasi kwamba watoto wake hawajui lugha nyingine zaidi ya Kijapani.

Katika video iliyosambaa mitandaoni baada ya mkutano uliofanyika Mei 13,mwaka huu, mfanyabiashara huyo alionekana akilia huku akihoji uamuzi wa mamlaka za uhamiaji kumtaka kurejea India baada ya kuishi nchini humo kwa miongo mitatu.

“Watoto wangu walizaliwa hapa,wako shule ya sekondari,wanazungumza Kijapani pekee na marafiki zao wote ni Wajapani. Nilifanya kazi kwa bidii hadi nikafanikiwa kununua nyumba. Inawezekanaje leo niambiwe nirudi India?,” alihoji Kumar kwa huzuni kubwa mbele ya hadhira.

Taarifa zinaeleza kuwa,matatizo yake yamechangiwa na sheria mpya za visa za wafanyabiashara zilizowekwa na serikali ya Japan mwaka 2025.

Chini ya sheria hizo mpya, waombaji wa visa za biashara wanatakiwa kuwa na mtaji wa angalau yen milioni 30 sawa na takribani Shilingi milioni 500 za Kitanzania, kiwango ambacho ni kikubwa mara sita zaidi ya kiwango cha awali cha yen milioni tano.

Serikali ya Japan imeeleza kuwa,hatua hiyo imelenga kudhibiti matumizi mabaya ya mfumo wa visa za biashara, baada ya kuibuka kwa taarifa kuwa baadhi ya wageni walikuwa wakitumia mfumo huo kupata makazi ya kudumu bila kuendesha biashara halali.

Hata hivyo, wakosoaji wa sera hiyo wanasema sheria hizo mpya zimewaathiri vibaya wageni wengi waliowekeza maisha yao nchini humo kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Japan, maombi ya visa za biashara yameshuka kwa karibu asilimia 96 tangu sheria hizo mpya zianze kutekelezwa.

Wamiliki wengi wa migahawa na biashara ndogo ndogo kutoka mataifa mbalimbali ya Asia wameanza kufunga biashara zao kutokana na kushindwa kukidhi masharti mapya ya kifedha.

Kesi ya Kumar imezua hisia kali mitandaoni huku maelfu ya watu wakisaini ombi la kutaka serikali ya Japan kupitia upya sheria hizo.

Wengi wameeleza kuwa,si haki kuwafukuza watu waliotumia sehemu kubwa ya maisha yao nchini humo, wamejenga familia, biashara na mahusiano ya kijamii ndani ya jamii ya Kijapani.

Kwa sasa, hatima ya Kumar pamoja na mgahawa wake aliouendesha kwa zaidi ya miaka 18 bado haijajulikana rasmi, huku suala hilo likiendelea kuzua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa wahamiaji wa muda mrefu nchini Japan.(NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here