Ubelgiji kujenga Kisiwa cha kwanza duniani cha nishati baharini kwa kuzamisha vizimba 23 vya zege vyenye uzito wa tani 22,000 kila kimoja

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Ubelgiji imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa kihandisi na nishati safi unaotarajiwa kubadili mfumo wa usambazaji wa umeme barani Ulaya, kwa kujenga kisiwa maalumu cha nishati katikati ya Bahari ya Kaskazini (North Sea), takribani kilomita 45 kutoka pwani ya nchi hiyo.
Picha na cpg.

Mradi huo unaojulikana kama Princess Elisabeth Island unatajwa kuwa wa kwanza duniani wa aina yake, ambapo vizimba vikubwa vya zege 23 vyenye uzito wa takribani tani 22,000 kila kimoja vitazamishwa baharini ili kuunda msingi wa kisiwa hicho kitakachokuwa kitovu cha kukusanya na kusafirisha umeme unaozalishwa na mashamba ya upepo yaliyopo baharini.

Kwa mujibu wa taarifa za kampuni ya usafirishaji wa umeme ya Elia pamoja na kampuni za ujenzi wa baharini za DEME na Jan De Nul, vizimba hivyo vya zege vitaunda ukuta wa nje wa kisiwa hicho kabla ya eneo la ndani kujazwa mchanga na miundombinu ya umeme wa msongo mkubwa.

Kisiwa hicho kinatarajiwa kuwa kitovu muhimu cha kuunganisha umeme kutoka mitambo ya upepo wa baharini na gridi kuu ya taifa ya Ubelgiji pamoja na nchi nyingine za Ulaya kupitia nyaya za chini ya bahari.

Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa,mradi huo utawezesha usafirishaji wa angalau gigawati 2.1 za umeme wa upepo kutoka Bahari ya Kaskazini, huku baadhi ya makadirio yakionesha uwezo wa kufikisha hadi gigawati 3.5 ikiwa ni kiwango kinachoweza kuhudumia zaidi ya nyumba milioni tatu barani Ulaya.

Mradi huo pia ni sehemu ya mkakati mpana wa Umoja wa Ulaya wa kuimarisha matumizi ya nishati jadidifu na kupunguza utegemezi wa mafuta na gesi asilia.

Kila kizimba cha zege kina urefu wa takribani mita 58, upana wa mita 28 hadi 30, na kimo kinachofikia mita 32 kulingana na muundo wake wa kinga dhidi ya mawimbi makubwa ya bahari.

Vizimba hivyo vinajengwa katika bandari ya Vlissingen nchini Netherlands kabla ya kusafirishwa baharini kwa kutumia meli kubwa za kuvuta mizigo.

Wataalamu wa ujenzi wa baharini wanasema operesheni ya kuvizamisha vizimba hivyo si ya kawaida, kwani kila kizimba hushushwa kwa umakini mkubwa kwa kutumia teknolojia za kisasa za upimaji na ufuatiliaji wa moja kwa moja ili kuhakikisha vinawekwa kwa usahihi wa hali ya juu chini ya bahari.

Takribani watu 150, meli 10 na boti nne kubwa za kuvuta mizigo zinashiriki katika kila hatua ya usafirishaji na usimikaji wa vizimba hivyo, huku kila operesheni ikichukua karibu saa 24 kukamilika kulingana na hali ya hewa na mawimbi ya bahari.

Baada ya ukuta wa nje kukamilika, eneo la ndani litajazwa zaidi ya mita za ujazo milioni 2.3 za mchanga ili kuandaa nafasi ya kufungwa kwa vifaa vya kusambaza umeme wa msongo mkubwa wa AC na DC kutoka kwenye mashamba ya upepo yaliyopo baharini.

Mradi huo pia utakuwa kituo cha kuunganisha nyaya za kimataifa za umeme kati ya Ubelgiji na mataifa mengine ya Ulaya kama vile Denmark na Uingereza, jambo linalotarajiwa kuongeza ushirikiano wa nishati katika bara hilo.

Mbali na uzalishaji wa nishati safi, wabunifu wa mradi huo wamejumuisha hatua maalumu za kulinda mazingira ya baharini.

Kwa mujibu wa Elia, sehemu za ukuta wa kisiwa hicho zimeundwa mahsusi kutoa maeneo ya kuzaliana na kupumzikia kwa ndege wa baharini pamoja na viumbe wengine wa majini.

Aidha, wataalamu wa mazingira wanatarajiwa kufanya ufuatiliaji wa muda mrefu ili kutathmini athari za mradi huo kwa mfumo wa ikolojia wa Bahari ya Kaskazini.

Wachambuzi wa sekta ya nishati wanautaja mradi wa Princess Elisabeth Island kama hatua kubwa katika mapinduzi ya nishati safi duniani, huku ukionesha jinsi teknolojia ya kisasa inavyoweza kutumiwa kuzalisha na kusafirisha umeme kwa ufanisi mkubwa kutoka baharini kwenda nchi mbalimbali za Ulaya.(clickpetroleoegas/NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here