Wabunge wakoleza kasi mageuzi Sekta ya Elimu nchini,wapendekeza mambo muhimu

NA GODFREY NNKO

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Mei 8,2026 limeendelea na mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/2027, huku wabunge wakijadili kwa kina masuala mbalimbali yanayohusu maboresho ya sekta ya elimu, ujumuishaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu,matumizi ya teknolojia pamoja na mageuzi ya mitaala nchini.
Bajeti hiyo iliwasilishwa bungeni Mei 7, 2026 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ambaye aliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 2.398 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo katika mwaka mpya wa fedha.

Katika mjadala huo, wabunge mbalimbali wametoa maoni, ushauri na mapendekezo wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha mfumo wa elimu ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia.

Pongezi mageuzi ya Sera ya Elimu

Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso (CCM) amesema,mabadiliko ya sera ya elimu yaliyofanywa chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan yameleta mafanikio makubwa katika sekta hiyo na kusaidia kuongeza usawa wa upatikanaji wa elimu nchini.
Akichangia mjadala huo bungeni, Pareso amesema,Serikali imefanya maboresho makubwa ya mitaala na mfumo wa elimu baada ya kuwepo kwa malalamiko ya muda mrefu kuhusu kutokidhi mahitaji ya wakati.

Pareso amesema,hatua ya Serikali kuruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kurejea shuleni imefungua fursa kwa maelfu ya watoto wa kike kuendelea na masomo yao baada ya awali kukatishwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ndoa za utotoni,umasikini na ukatili wa kijinsia.

Kwa mujibu wa Pareso, takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya wanafunzi 4,000 walikuwa wakikatisha masomo kutokana na changamoto hizo, jambo lililosababisha Serikali kufanya maboresho ya sera ya elimu ili kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu bila ubaguzi.

Ameongeza kuwa, hadi sasa zaidi ya wanafunzi 10,000 wamerejeshwa shuleni, hatua aliyosema inaonesha dhamira ya Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha elimu inakuwa jumuishi kwa wote.

Aidha, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuimarisha elimu ya ufundi na stadi za kazi kupitia ujenzi wa vyuo vya VETA nchini kote, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuwawezesha vijana kupata ujuzi na kuongeza nafasi za ajira.

Matumizi ya Akili Unde

Naye Mbunge wa Jimbo la Msalala mkoani Shinyanga,Mabula Magangila ameishauri Serikali kuanza kutumia teknolojia ya Akili Unde (AI) kufundishia baadhi ya masomo ili kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa walimu nchini.
Magangila amesema,mabadiliko ya mtaala yanatarajiwa kuongeza idadi kubwa ya wanafunzi shuleni ifikapo mwaka 2028, hali inayoweza kusababisha msongamano mkubwa kama maandalizi ya kutosha hayatafanyika mapema.

Amesema,mfumo mpya wa elimu utahitaji zaidi ya walimu 40,000, hivyo Serikali inapaswa kuwekeza mapema katika miundombinu ya elimu pamoja na mbinu mbadala za ufundishaji.

Mbunge huyo amesema, endapo walimu hawatatosha, baadhi ya mada zinaweza kufundishwa kwa kutumia teknolojia ya AI ili kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kupata elimu kwa wakati.

Elimu Jumuishi

Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha Wanawake wenye Ulemavu, Nassriya Nassir Ali ameitaka Serikali kujenga shule jumuishi katika kila mkoa ili kupunguza changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu kusafiri umbali mrefu kutafuta elimu maalumu.

Amesema,watoto wengi wenye ulemavu bado wanapata ugumu kupata huduma za elimu karibu na maeneo wanayoishi.

Mbunge huyo ametolea mfano maisha yake binafsi ambapo alilazimika kutoka Zanzibar kuja kusoma Tanzania Bara kutokana na uhaba wa huduma hizo.

Pia amependekeza lugha ya alama ifundishwe rasmi kuanzia shule za msingi ili kuongeza ujumuishaji katika mfumo wa elimu na kurahisisha mawasiliano kwa watu wenye uziwi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, wadau wa elimu maalumu pamoja na vyama vya watu wenye ulemavu wakati wa kuandaa sera, mitaala na miongozo ya elimu.

Katika mchango wake, Nassriya amesema watu wenye ulemavu, hususan wenye changamoto ya uziwi, hukabiliwa na mazingira magumu ya ujifunzaji jambo linalowalazimu kutumia muda mrefu zaidi kumaliza masomo yao.

Pia ameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya shule, kuongeza walimu wa elimu maalumu na kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanajumuishwa katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili waweze kupata huduma muhimu za afya.

Vilevile, ameiomba Wizara ya Elimu kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika sekta ya elimu maalumu, akisema bado kuna changamoto kubwa katika utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu Zanzibar.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Stella Ikupa (CCM) ameishauri Serikali kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa watu wenye ulemavu kwa mfumo wa ruzuku ili kuwawezesha kupata elimu kwa urahisi zaidi.

Ikupa amesema,kuna umuhimu wa walimu wote nchini kupewa mafunzo ya elimu maalumu ili kurahisisha ujumuishaji wa wanafunzi wenye ulemavu katika shule za kawaida.

Aidha,amependekeza shule za mabweni zinazohudumia wanafunzi wenye ulemavu kuwa na wasaidizi maalumu wa kuwahudumia wanafunzi hao ili waweze kusoma katika mazingira rafiki na salama.
Mbunge huyo pia amependekeza kuanzishwa kwa Bodi au Mamlaka ya Elimu Jumuishi ili kusimamia kikamilifu masuala ya elimu kwa watu wenye mahitaji maalumu.

Makambi ya Wanafunzi

Naye Mariam Ditopile Mzuzuri ambaye ni mbunge wa Jimbo la Kondoa amesema, kuanzishwa kwa makambi maalumu kwa wanafunzi wa shule za kutwa kumechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha ufaulu wa wanafunzi hao na kupunguza tofauti ya matokeo kati ya shule za kutwa na za bweni.

Amesema,mfumo huo umeleta mafanikio makubwa katika Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma kwa kuwapatia wanafunzi mazingira bora ya kujisomea na kujiandaa kwa mitihani.

Kutokana na hali hiyo, Mariam ameitaka Serikali pamoja na wadau wa elimu kusaidia makambi hayo kwa kuyapatia mahitaji muhimu yatakayowezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora zaidi.

Katika hatua nyingine, amempongeza Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda pamoja na Naibu Waziri, Wanu Hafidh Ameir kwa usimamizi mzuri wa sekta ya elimu nchini.

Elimu ya Vitendo na Teknolojia

Mbunge wa Viti Maalum, Fatma Rembo ameishauri Serikali kufanya mageuzi ya mfumo wa elimu kwa kuhamia zaidi kwenye elimu ya vitendo badala ya kutegemea nadharia pekee.

Amesema,mfumo wa elimu unapaswa kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na kuwasaidia kujiajiri au kuajirika kwa haraka baada ya kuhitimu masomo yao.
Pia, amesema ongezeko la vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) kutoka 1,414 mwaka 2025 hadi 1,446 mwaka 2026 ni hatua muhimu katika kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea.

Mbunge huyo pia alipendekeza masomo ya Coding, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na maadili kuanza kufundishwa tangu elimu ya msingi ili kuandaa kizazi chenye uwezo wa kuhimili ushindani wa dunia ya kidijitali.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya vyuo vya ufundi na sekta ya viwanda ili kupunguza pengo la ujuzi kwa wahitimu wanaoingia kwenye soko la ajira.

Uzalendo kwa Vijana

Mbunge wa Viti Maalum, Zainab Abdallah amesema,kuna umuhimu wa vijana wa kizazi cha Gen Z kupewa mafunzo ya ukakamavu na uzalendo kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kuwajengea nidhamu, uzalendo na moyo wa kulitumikia taifa.

Akichangia mjadala huo amesema, vijana wengi wa kizazi hicho wanahitaji kuimarishwa katika misingi ya utaifa na uzalendo.

Mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia unaendelea huku wabunge wengi wakielekeza hoja zao katika kuboresha ubora wa elimu, kuongeza usawa wa upatikanaji wa huduma za elimu na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji.
Profesa Mkenda amesema, katika mwaka wa fedha 2026/2027, wizara imeandaa vipaumbele vyake kwa kuzingatia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, inayolenga kuimarisha ubora wa elimu, kukuza ujuzi na kuongeza maarifa kwa wananchi.

Amesema,serikali itaendelea kuweka mkazo katika maandalizi ya utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), pamoja na kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuendana na mahitaji ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Wizara imejielekeza katika utekelezaji wa vipaumbele vitano vikuu ambavyo ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala,kufanya mapitio ya sheria, kuandaa miongozo na kutoa mafunzo.
Pili,kuongeza fursa na kuboresha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya amali na tatu ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu.

Nne ni kuongeza fursa na kuboresha ubora wa elimu ya juu na tano ni kuimarisha uwezo wa taifa katika tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa lengo la kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here