DAR-Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-CENTRE) kimesema kampuni ya mabasi yaendayo haraka ya Mofat inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maeneo ya kutoa huduma, hali iliyosababisha zaidi ya mabasi 150 kubaki yameegeshwa tangu yaliponunuliwa, huku mabasi 50 pekee yakiendelea kutoa huduma kwa abiria.
Akizungumza Mei 6, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa PPP-CENTRE, David Kafulila alisema changamoto hiyo imeathiri utekelezaji wa mradi huo wa ubia kati ya DART na Mofat ambao sasa una miezi sita tangu kuanza kwake.
Kafulila alisema,walifanya ziara ya kukagua mradi huo pamoja na wadau wa sekta binafsi kwa lengo la kutathmini maendeleo yake na kubaini changamoto zinazoukabili. Alieleza kuwa Serikali ina wajibu wa kufuatilia miradi yote ya ubia kuanzia hatua za mwanzo hadi mwisho ili kuhakikisha uwekezaji unaendelea kuwa na tija.
Aidha, alisema kukwama kwa mabasi hayo kwa zaidi ya nusu mwaka kunasababisha hasara kwa mwekezaji, hivyo akaishauri kampuni hiyo kuandaa ripoti ya tathmini ya utekelezaji wa mradi kwa kipindi cha miezi sita ili iweze kuwasilishwa Serikalini kwa ajili ya maboresho na ufumbuzi wa changamoto zilizopo.
Kwa upande wake, Msemaji wa kampuni ya Mofat, Philip Changala alisema mradi huo ni wa muhimu kwa wananchi wa Dar es Salaam, hasa wakazi wa maeneo ya Mbagala, Kivukoni na Gerezani, kutokana na mahitaji makubwa ya huduma ya usafiri.
Changala alisema,ziara ya PPP-CENTRE imeonesha dhamira ya Serikali ya kusikiliza changamoto za wawekezaji binafsi na kuboresha mazingira ya biashara. Pia aliipongeza TPSF kwa mchango wake wa kuwasilisha changamoto za sekta binafsi Serikalini huku akibainisha kuwa kampuni hiyo itaendelea kubuni huduma mbalimbali za usafiri ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
