Wafanyakazi wa benki wauawa kwa kupigwa risasi

NA DIRAMAKINI

WAFANYAKAZI wawili wa benki wameuawa kwa kupigwa risasi baada ya tukio la uporaji wa benki kugeuka kuwa mauaji ya kikatili katika jimbo la Kentucky,Marekani huku vyombo vya usalama vikiendelea na msako mkali wa kumtafuta mshukiwa aliyekimbia.
Kwa mujibu wa Polisi wa Jimbo la Kentucky, tukio hilo lilitokea Alhamisi mchana majira ya saa nane katika tawi la benki ya U.S. Bank lililopo mtaa wa Chestnut, mjini Berea.

Mshukiwa, anayedaiwa kuwa na silaha na kuvaa barakoa, aliingia ndani ya benki hiyo na kufyatua risasi zilizowalenga wafanyakazi wawili ambapo mwanaume na mwanamke walifariki dunia papo hapo.

Maafisa wa usalama wamesema, baada ya shambulio hilo, mshukiwa alitoroka eneo la tukio na kuacha hofu kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Polisi wamemtaja mshukiwa kuwa mtu hatari, aliyekuwa amevalia fulana yenye kofia ya rangi nyepesi, glavu nyeusi, suruali ya kijivu na viatu vya michezo vya rangi nyepesi.

Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa Polisi wa Jimbo hilo, Trooper Scottie Pennington amesema, tukio hilo limewaacha wananchi katika hali ya hofu na taharuki, huku akisisitiza juhudi za dhati za kumkamata mtuhumiwa huyo.

“Tunatambua wananchi wana hofu, nasi pia tuna hofu kwa ajili yao. Tutaendelea kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha anapatikana na kufikishwa mbele ya sheria,”amesema.

Msako mkubwa unaendelea ukihusisha vyombo mbalimbali vya usalama, ikiwemo mashirika ya shirikisho, huku mbinu za kisasa kama ndege zisizo na rubani (drones), mbwa wa upelelezi na upekuzi wa nyumba kwa nyumba zikitumika kumtafuta mshukiwa huyo.

Kutokana na tukio hilo, baadhi ya taasisi za elimu katika eneo hilo zililazimika kufungwa kwa muda kama hatua ya tahadhari, huku wananchi wakitakiwa kutoa taarifa yoyote itakayosaidia uchunguzi unaoendelea.

Mamlaka zimeendelea kutoa wito kwa umma kutojaribu kumkaribia mshukiwa iwapo ataonekana, bali kutoa taarifa kwa vyombo vya dola mara moja, huku zikisisitiza kuwa usalama wa wananchi ni kipaumbele kikuu wakati operesheni ya msako ikiendelea.(NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here