NA DIRAMAKINI
MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Tilisho, Bw. John Tilisho, hatimaye amezungumza hadharani kwa mara ya kwanza kufuatia uvumi uliokuwa ukienea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu madai ya kuwepo kwa mgogoro kati yake na mfanyakazi wake anayejulikana kama Nayce Moshi.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Bw. Tilisho amekanusha vikali taarifa hizo, akieleza kuwa hakuna mgogoro wowote uliowahi kutokea kati yake na mhusika huyo, kinyume na madai yaliyokuwa yakisambazwa na baadhi ya watumiaji wa mitandao.
Katika maelezo yake, amefafanua kuwa Nayce Moshi aliomba ruhusa ya kupumzika kwa muda ili kujikita katika shughuli zake binafsi za kibiashara, ombi ambalo alilikubali kwa hiari.
Aidha, amebainisha kuwa walifikia makubaliano ya wazi kwamba baada ya mhusika huyo kuimarisha biashara zake, atarejea kazini kama kawaida.
“Ni muhimu kwa jamii kujenga utamaduni wa kuheshimu taarifa sahihi na kuepuka kueneza uvumi usio na uthibitisho,” amesisitiza Bw. Tilisho, akiongeza kuwa ni vyema watu kuhakikisha wanapata ukweli kutoka kwa wahusika kabla ya kutoa au kusambaza taarifa zinazoweza kupotosha umma.
Kauli hiyo ya kiongozi huyo wa Tilisho imekuja wakati ambapo kumekuwepo na ongezeko la taarifa zisizo rasmi mitandaoni, hali inayochochea mjadala mpana kuhusu uwajibikaji katika matumizi ya majukwaa ya kidijitali.
Pia,ametoa wito kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kuzingatia maadili ya mawasiliano, ikiwa ni pamoja na kuheshimu faragha na hadhi ya watu wengine, pamoja na kuthibitisha ukweli wa taarifa kabla ya kuzisambaza.
