NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linaendelea na uchunguzi wa kina kufuatia tukio la mauaji ya Bw. James Rogers Temba, mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM), aliyekutwa amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.
Mwili wa marehemu uligunduliwa Aprili 30, 2026 ukiwa unaelea katika maji ya Mto Msimbazi eneo la Kipawa, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mwili huo ulikuwa hauna kichwa, hali iliyozua hofu na taharuki miongoni mwa wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Mei 6, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro amesema kuwa, tayari watu wanne wanashikiliwa kuhusiana na tukio hilo, huku uchunguzi zaidi ukiendelea ili kubaini ukweli wa tukio hilo pamoja na mtandao unaoweza kuhusika.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Steven Chaka (31), afisa maabara na mkazi wa Bomang’ombe wilayani Hai mkoani Kilimanjaro; Anna Frank Lema (30), mfanyabiashara na mkazi wa Tabata Chang’ombe, Dar es Salaam; Twalibu Khamis Mpulo (23) mkazi wa Kigogo Kati; pamoja na Michael John (26) mkazi wa Kigogo, jijini humo.
Kamanda Muliro alibainisha kuwa, jeshi hilo pia linashikilia vielelezo mbalimbali vinavyofanyiwa uchunguzi wa kisayansi ili kusaidia kufanikisha hatua za kisheria dhidi ya wahusika wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo.
Amesisitiza kuwa, uchunguzi unaendelea kwa umakini mkubwa, na kwamba hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika, kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu na kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zozote zitakazoweza kusaidia uchunguzi, huku likiahidi kutoa taarifa zaidi kadri uchunguzi utakavyoendelea.
