Waziri wa Fedha afungua mkutano wa Kimataifa wa forodha Zanzibar

ZANZIBAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amelishauri Baraza la Uongozi la Shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA), kuja na mwarobaini wa kukabiliana na changamoto zinazokwaza ufanisi wa ufanyaji biashara ya kimataifa miongoni mwa nchi wanachama wa Baraza hilo.
Mhe. Balozi Omar amesema hayo wakati akifungua rasmi Mkutano wa 32 wa Baraza la Uongozi la Shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Golden Tulip iliyopo karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume-Zanzibar.
Alionesha wasiwasi wake juu ya ongezeko la biashara ya mtandaoni, maendeleo ya teknolojia ikiwemo unde, big data, na changamoto za kiusalama zinazoathiri biashara ya kimataifa na alilitaka baraza hilo kuchukua jukumu la kuimarisha ushirikiano na kukuza taasisi za kisasa za forodha.
Mhe. Balozi Omar alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia mifumo ya kisasa ya kidijitali, usimamizi wa vihatarishi pamoja na matumizi ya teknolojia za ukaguzi ili kuongeza ufanisi katika udhibiti wa mipaka na ukusanyaji wa mapato.
Akitaja Dira ya Maendeleo 2050, Mhe. Balozi Omar alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa na ujumuishaji wa mifumo ili kuendeleza biashara na kuvutia Uwekezaji wa Moja kwa Moja wa Nje (Foreign Direct Investment -FDI).

“Nina wahimiza wajumbe kutumia jukwaa la mkutano huu kuimarisha ushirikiano, kubadilishana maarifa na kutafuta suluhu za vitendo na nina wahimiza wageni kutembelea vivutio vya Tanzania ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Serengeti na Zanzibar,”alisema Mhe. Balozi Omar.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda, ameeleza kuwa TRA imeendelea kufanya maboresho makubwa ya mifumo ya forodha kupitia uwekezaji katika mifumo ya kidijitali, uimarishaji wa mifumo ya usimamizi wa mizigo pamoja na kuunganisha huduma za forodha katika dirisha moja la utoaji huduma kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na kurahisisha biashara.
Mkutano huo wa 32 wa Baraza la Uongozi la Shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA), unawakutanisha Wanachama kutoka Mataifa 24 na kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa forodha, mageuzi ya kidijitali, usalama wa mipaka, uboreshaji wa biashara na namna bora ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya forodha duniani huku ukilenga kuimarisha ustawi wa uchumi wa nchi wanachama wa ukanda huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here