NA LWAGA MWAMBANDE
LEO Watanzania wameungana na jamii mbalimbali kuadhimisha Siku ya Mama Duniani,kwa lengo la kuthamini na kutambua mchango mkubwa wa akina mama katika malezi ya familia na maendeleo ya jamii.
Maadhimisho haya yameambatana na wito wa kuendelea kulinda haki za wanawake, kuwainua kiuchumi na kuhakikisha wanapata mazingira bora ya maisha.
Kwa kutambua umuhimu wa siku hii, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande amesisitiza kuwa, mama ni nguzo muhimu katika familia na taifa kutokana na nafasi yao katika malezi,maadili na ustawi wa jamii, hivyo ni kila kitu.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwainua wanawake kiuchumi na kielimu ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Aidha, elimu kuhusu afya ya uzazi, ulinzi dhidi ya ukatili wa kijinsia pamoja na upatikanaji wa huduma bora za afya kwa mama na mtoto iendelee kupewa kipaumbele. Endelea;
1. Mama kila kitu mama, wewe vyote wapokea,
Mema kama yaja mama, nyumbani wayapokea,
Mabaya yakija mama, huna kwa kuyatolea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
2. Tunaposema uzazi, mama twakuongelea,
Ukipata ile dozi, wana watubebea,
Mimba kubeba ni kazi, ni mengi yanatokea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
3. Chakula unachopenda, puani chakutokea,
Mwendo unaopenda, na mimba wapotea,
Shepu inayokuranda, mbali yatelezea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
4. Malezi watoto wako, mama yanakungojea,
Hata baba akiweko, zigo lakuelemea,
Kama shida zikiwako, wewe zakuegemea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
5. Huzuni ikitokea, ni mama unatokea,
Majonzi watubebea, mbele tunaendelea,
Hadi tunapokomea, wewe unaendelea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
6. Kama chereko chereko, ili zipate nogea,
Mama macho yetu kwako, jinsi unapendezea,
Na madikodiko huko, wewe unatutolea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
7. Mama una siri nyingi, yale tunakutendea,
Kwako jambo la msingi, kifua unapokea,
Unayomezea mengi, kisema tungepotea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
8. Kuwaombea wababa, kazi inaendelea,
Mama hiyo umeshiba, mbele wanaendelea,
Kila kona unakaba, Mungu anatutendea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
9. Asubuhi na mapema, wewe unatokezea,
Ili mambo yawe mema, wengine tukitokea,
Wewe mwingi wa huruma, jinsi unajitolea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
10. Mama ulipofikia, hili nakuelezea,
Tafadhali saidia, mabinti zako kulea,
Ili waweze fikia, kazi wakakupokea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
11. Na watoto wa kiume, vema kuwaelezea,
Wafanye mambo kiume, majukumu kupokea,
Kesho waje wasimame, kizazi kuendelea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
12. Leo ni siku ya mama, heri tunakutolea,
Epukana na dhahama, mbele ukiendelea,
Vema uweze simama, kazi ikiendelea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
13. Kujengeka familia, taifa kuendelea,
Mama twakuangalia, kazi njema endelea,
Usije ukasinzia, dunia italegea,
Hongera kwa siku yako, wewe kila kitu mama.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)