DODOMA-Wizara ya Afya na Taasisi ya Kimataifa ya Living Goods ya Nchini Marekani zimekutana leo Jijini katika kikao cha pamoja Jijini Dodoma kujadiliana namna bora ya ushiriki wa Taasisi hiyo kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha Afua za Huduma za Afya Ngazi ya Jamii Nchini.
Taasisi ya Living Goods imejikita katika juhudi za kuokoa maisha kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha watoa huduma za afya ngazi jamii wanafanya kazi kidijitali, wakiwezeshwa ipasavyo kutoa huduma kila wanapohitajika.
Kikao hicho kimefanyika Makao Makuu ya Wizara ya Afya leo tarehe 7, Mei 2026 Jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Huduma za Kinga Dkt. Otilia Gowele ambaye ameutaka ujumbe wa Taasisi hiyo kuagazia maeneo mengine ya uwezeshaji kiwemo kuwaendeleza wahudumu wa afya ngazi ya jamii kielimu na kiuchumi.
Aidha Kiongozi huyo amesema tayari serikali ina kazi zinazoendelea kuhusu Huduma za Afya ngazi ya jamii hivyo kuitaka Taasisi hiyo kuangalia masuala yanayotekelezwa na serikali ili kubaini mwanya utakaowaezesha kuangazia maeneo zaidi ya ushirikiano.
Naye Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Huduma za Kinga Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Dkt. Rahama Hingora amewambia ujumbe wa Taasisi hiyo kuwa umekuja wakati muhafaka kwani serikali inatekeleza afua kama hizo ambazo bado zinahitaji ushirikiano mkubwa kuboresha huduma za Afya Ngazi ya Jamii.
Wakati huo Mratibu wa Programu ya Huduma za Afya Ngazi ya Jamii Dkt. Norman Kyara kutoka Wizara ya Afya wakati aikiwasilisha mada yake amesema sula la kuwezesha huduma za afya kidijitali linaendelea kufanyiwa kazi na serikali hivyo ujio wa Taasisi hiyo umekuja kwa wakati sahihi ili kuhimarisha juhudi za serikali zilizopo katika utekelezaji wa afua hiyo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Teknolijia na Uhandisi wa Shirika hilo Bi. Hilda Ngondoki amesema Taasisi yake inatoa huduma kwa kushirikiana na serikali ambazo tayari Taasisi hiyo inatoa huduma kupitia mtandao wake wa wadau ikiwemo huduma za kifedha hivyo inaangazia zaidi kupata ushirikiano kutoka kwa serikali.











