NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) inatangaza bei mpya za tiketi za boti kwa daraja la chini (Economy Class) zitakazoanza kutumika kuanzia siku ya Jumatatu ya Mei 11,2026.
Daraja la chini (Economy) bei ya zamani ilikuwa shilingi 35,000 kwa mtu mzima na bei mpya itakuwa ni shilingi 40,000 huku kwa watoto daraja la chini nusu ya bei ya tiketi ni shilingi 20,000.Abiria waliokuwa wanapanda kwa bei ya Shilingi 20,000 itakuwa shilingi 22,000 huku watoto watalipa shilingi 11,000.
Katika taarifa hiyo ya mamlaka imesema,bei hizi mpya ni kwa ajili ya boti za abiria ziendazo kwa kasi pamoja na Boti ya Flying Horse tu na hazitahusisha meli za mizigo na abiria ziendazo taratibu (Passenger cargo Ships).
Sababu za kupanda kwa bei ya tiketi, ni kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na kuongezeka kwa bei za uagizaji vipuri kutoka nje ya nchi kuja Tanzania.
Aidha,mamlaka inawataka wamiliki wa vyombo kuzingatia bei hizi, na pia inawaomba wananchi kununua tiketi katika Ofisi za kampuni au Wakala wanaotambulika na kuacha kununua tiketi za ulanguzi.
Mamlaka imewaomba wananchi kutoa ushirikiano iwapo chombo chochote kitakwenda kinyume na bei elekezi zilizoidhinishwa na mamlaka.