Wizara ya Elimu yaomba shilingi Trilioni 2.398 kwa Bajeti ya 2026/27 kutekeleza vipaumbele vikuu vitano

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 2.398 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo pamoja na miradi mbalimbali ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2026/2027, huku ikielekeza nguvu katika maboresho ya mfumo wa elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu nchini.
Makadirio hayo yamewasilishwa bungeni jijini Dodoma leo Mei 7,2026 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akiwasilisha hotuba ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Profesa Mkenda amesema, kati ya fedha zote zilizoombwa, kiasi cha Shilingi 2,394,423,829,000 ni kwa ajili ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Fungu 46), ambapo Shilingi 697,841,881,000 zimeelekezwa kwenye matumizi ya kawaida.

Amefafanua kuwa, ndani ya fedha za matumizi ya kawaida, Shilingi 648,082,352,000 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi, huku Shilingi 49,759,529,000 zikielekezwa kwenye matumizi mengineyo ya kiutendaji.

Aidha, Waziri Mkenda amesema kiasi cha Shilingi 1,696,581,948,000 kinaombwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kati ya fedha hizo, Shilingi 1,337,249,000,000 ni fedha za ndani, huku Shilingi 359,332,948,000 zikitarajiwa kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda amesema,wizara kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO (Fungu 18) imeomba kuidhinishiwa Shilingi 3,866,993,000 kwa matumizi ya kawaida.

Amesema,kati ya fedha hizo, Shilingi 1,335,020,000 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi, huku Shilingi 2,531,973,000 zikielekezwa kwenye matumizi mengineyo ya uendeshaji wa shughuli za tume hiyo.
Vipaumbele vya Bajeti 2026/27

Profesa Mkenda amesema, katika mwaka wa fedha 2026/2027, wizara imeandaa vipaumbele vyake kwa kuzingatia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, inayolenga kuimarisha ubora wa elimu, kukuza ujuzi na kuongeza maarifa kwa wananchi.

Amesema,serikali itaendelea kuweka mkazo katika maandalizi ya utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), pamoja na kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuendana na mahitaji ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Wizara imejielekeza katika utekelezaji wa vipaumbele vitano vikuu ambavyo ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala,kufanya mapitio ya sheria, kuandaa miongozo na kutoa mafunzo.

Pili,kuongeza fursa na kuboresha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya amali na tatu ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu.

Nne ni kuongeza fursa na kuboresha ubora wa elimu ya juu na tano ni kuimarisha uwezo wa taifa katika tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa lengo la kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Akizungumzia utekelezaji wa sera na mitaala, Profesa Mkenda amesema, Serikali itafanya tathmini ya miaka miwili ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023 ambayo ilianza kutekelezwa Januari 2024 na kuzinduliwa rasmi Februari 1, 2025.

Amesema,lengo la tathmini hiyo ni kubaini mafanikio yaliyopatikana hadi sasa pamoja na changamoto zinazokwamisha utekelezaji wake ili kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha sekta ya elimu.

Pia,Serikali itaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10, hatua inayolenga kuwezesha wanafunzi wa darasa la sita na la saba kuanza kupokelewa kwa wakati mmoja kuanzia Januari 2028.

Profesa Mkenda amesema, utekelezaji wa mpango huo unasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, huku Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikishirikiana katika maandalizi ya miongozo, upatikanaji wa rasilimali za ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa muhimu, pamoja na utoaji wa mafunzo kwa walimu.

Waziri huyo amesema, serikali pia itakamilisha mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 ili kuendana na mabadiliko ya sera na mahitaji ya sasa ya sekta ya elimu.

Aidha, mapitio yatafanyika katika sheria zinazosimamia taasisi zilizo chini ya wizara hiyo zikiwemo Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) pamoja na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Amesema,hatua hiyo inalenga kuhakikisha taasisi hizo zinaendana na mabadiliko ya sera, sheria pamoja na makubaliano ya kikanda na kimataifa.

Katika kuimarisha mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu katika maendeleo ya taifa, Profesa Mkenda amesema,serikali itakamilisha mapitio ya Sera ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1996 ili kuangalia kama bado inakidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Amesema,mapitio hayo yatawezesha nchi kuwa na sera imara ya kusimamia masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu kulingana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa pamoja na mahitaji ya kikanda na kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here