NA GODFREY NNKO
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema kuwa,ndani ya siku 100 tangu kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan tayari imeanza kutekeleza mageuzi makubwa ya sekta ya elimu yenye lengo la kuimarisha ubora wa ujifunzaji na kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani na kimataifa.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 7, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Profesa Mkenda amesema kuwa,katika kipindi hicho kifupi tangu kuapishwa kwa Rais Dkt Samia, Serikali imeonesha dhamira ya dhati ya kufanya mageuzi ya kimkakati katika sekta ya elimu ili kujenga mfumo imara wa kuzalisha wahitimu wenye maarifa, ujuzi wa kujitegemea na uwezo wa kushindana katika uchumi wa dunia.
Amesema,moja ya hatua muhimu zilizochukuliwa ni kuandaliwa kwa Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali pamoja na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mpango huo ulizinduliwa rasmi Januari 29, 2026 jijini Dar es Salaam na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ukiwa na lengo la kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayefika darasa la tatu bila kuwa na uwezo wa msingi wa kusoma, kuandika na kuhesabu.
“Mpango huu ni hatua ya kimkakati katika kuboresha elimu ya msingi na kujenga msingi thabiti wa ujifunzaji kwa watoto wetu tangu hatua za awali,”amesema Profesa Mkenda.
Aidha, Waziri huyo amesema Serikali imeandaa mpango wa pamoja unaowakutanisha waajiri, vyuo vya elimu ya ufundi stadi pamoja na vyuo vikuu kwa lengo la kuoanisha mafunzo yanayotolewa na mahitaji halisi ya soko la ajira.
Mpango huo ulizinduliwa Februari 9, 2026 jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Emmanuel John Nchimbi.
Profesa Mkenda ameeleza kuwa,mpango huo unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya ajira, viwanda na taasisi za elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo kwa vitendo sambamba na kuandaliwa kwa wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika mazingira ya sasa ya kazi.
Ameongeza kuwa,Serikali ina matumaini makubwa kuwa ushirikiano huo utaongeza fursa za ajira kwa wahitimu, kuimarisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na kupunguza changamoto ya kutokuwapo kwa uwiano kati ya ujuzi wa wahitimu na mahitaji ya waajiri.
“Lengo letu ni kuona elimu inakuwa kichocheo cha maendeleo ya uchumi kwa kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa kwa ufanisi,”amesisitiza Waziri Mkenda.
Hatua hizo zinaelezwa kuwa,sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha sekta ya elimu nchini na kuifanya iwe na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa viwanda, ubunifu na ushindani wa kimataifa.






