NA GODFREY NNKO
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt.Asha Rose Migiro amesema chama hicho kilipokea kwa masikitiko makubwa matukio yaliyojitokeza Oktoba 29, 2025 na kusababisha vifo,majeruhi pamoja na taharuki kubwa nchini.
Akizungumza katika mahojiano maalum leo Mei 28,2026 kupitia kipindi cha Kasiri la Kikeke cha Crown FM, Dkt.Migiro amesema,tukio hilo lilikuwa la kushtua kwa Watanzania wengi na hasa wanachama wa CCM, akieleza kuwa halijawahi kutokea katika historia ya taifa hili lenye sifa ya amani, utulivu na mshikamano kwa miaka mingi.
“29 Oktoba 2025 ni tukio ambalo lilishtua wengi, na sisi wana CCM tulishtuka zaidi. Haijawahi kutokea katika Taifa letu,”amesema Dkt. Migiro.
Ameeleza kuwa,baada ya tukio hilo, chama kilihitaji muda wa kulitafakari kwa kina pamoja na kupitia taarifa iliyotolewa na Tume iliyoongozwa na Jaji Othman Chande kuhusu kilichotokea na namna taifa linavyoweza kuepuka kurudia hali kama hiyo siku zijazo.
Kwa mujibu wa Dkt. Migiro,CCM iliunga mkono kuundwa kwa tume hiyo na kuthamini kazi iliyofanywa na wajumbe wake kwa weledi mkubwa.
Amesema,chama hicho pia kinawapongeza wananchi kwa kujitokeza kutoa ushahidi na maoni yaliyosaidia kukamilika kwa uchunguzi huo.
Katibu Mkuu huyo amesema,kwa sasa CCM imeona ni wakati mwafaka kuzungumza kwa kina kuhusu msimamo wake juu ya taarifa ya tume pamoja na hatua zinazopaswa kufuatwa baada ya uchunguzi huo.
“Tumeipokea taarifa hii kwa umakini mkubwa kwa sababu tunataka kujua nini kilitokea na kwa nini kilitokea ili jambo kama hili lisijirudie tena,” amesema.
Katika maelezo yake, Dkt.Migiro amesema,CCM inaendelea kusikitishwa na idadi ya watu waliopoteza maisha kufuatia matukio hayo, akirejea taarifa ya Jaji Chande iliyobaini kuwa watu takribani 518 walifariki dunia pamoja na wengine kujeruhiwa au kupata madhara mbalimbali.
Amesema,chama hicho hakina sababu ya kutilia shaka takwimu zilizotolewa na tume kwa kuwa zilipatikana kupitia hospitali za Serikali, hospitali binafsi pamoja na taarifa za Msajili wa Vizazi na Vifo, ingawa tume ilieleza uwezekano wa idadi hiyo kubadilika kutokana na baadhi ya watu kutowasilisha taarifa rasmi.
“Kwa Chama Cha Mapinduzi, uhai wa mtu mmoja ni jambo kubwa sana ambalo haliwezi kupimwa kwa namba,” amesema.
Akizungumzia nafasi ya vyombo vya ulinzi na usalama katika tukio hilo, Dkt. Migiro amesema, taasisi hizo zilikuwa zikitekeleza wajibu wake wa msingi wa kulinda usalama wa wananchi na mali zao pamoja na kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unaendelea katika vituo mbalimbali vya kupigia kura nchini.
Ameeleza kuwa,siku hiyo kulikuwa na takribani vituo 90,000 vya kupigia kura nchi nzima, huku vyombo vya usalama vikilazimika kugawanyika kukabiliana na vurugu zilizozuka katika maeneo mbalimbali nchini wakati huo huo vikihakikisha usalama katika vituo vya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, fujo zilizotokea zilienea katika maeneo mengi nchini na si jijini Dar es Salaam pekee, hali iliyosababisha vyombo vya usalama kuwa na jukumu kubwa la kuzuia madhara zaidi yasitokee.
Amesema,CCM inavipongeza vyombo hivyo kwa kazi yao ya kulinda amani na utulivu wa taifa katika kipindi hicho kigumu, huku akisisitiza kuwa pongezi hizo hazimaanishi kupuuza dosari zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
“Kuna uwezekano wa kuwepo dosari katika utendaji wao, lakini hilo haliondoi ukweli kwamba walifanya kazi kubwa ya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama,” amesema.
Aidha, Dkt. Migiro amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuchunguza mazingira yaliyosababisha vifo hivyo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa huku taifa likijifunza namna bora ya kuimarisha amani, mshikamano na utulivu wa nchi siku zijazo.