DAR-Zikiwa zimesalia siku chache kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Benki Kuu hiyo iliandaa Bonanza la Michezo lililosheheni michezo mbalimbali ikiwemo riadha, mpira wa miguu, mpira wa pete na mpira wa kikapu.
Bonanza hilo lilifanyika tarehe 6 Juni 2026 katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha wafanyakazi wa Benki Kuu pamoja na wadau mbalimbali.
BoT inatarajia kuadhimisha rasmi miaka 60 tangu kuanzishwa kwake tarehe 14 Juni 1966, katika hafla itakayofanyika tarehe 12 Juni 2026 kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa Bonanza hilo, Mgeni Rasmi ambaye pia ni Naibu Gavana wa BoT anayesimamia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, alisema kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha afya, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi.
Alieleza kuwa mshikamano unaojengwa kupitia matukio ya michezo huchangia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi, jambo ambalo lina mchango mkubwa katika kukuza na kustawisha uchumi wa nchi.
Bonanza hilo ni sehemu ya shughuli mbalimbali zinazoendelea kufanyika kuelekea katika kilele cha maadhimisho hayo, yanayobeba kaulimbiu ya ‘Miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania: Uchumi Imara na Endelevu’.











