DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uhuru wa kiuchumi wa Tanzania tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966, ikihakikisha uthabiti wa bei, uimara wa sekta ya fedha, na maendeleo ya mifumo ya malipo nchini.
Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 12 Juni 2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema mafanikio hayo yanaakisi mchango mkubwa wa taasisi hiyo katika kulindda na kuendeleza uchumi wa taifa kwa miongo sita.

Rais Samia alikumbusha kuwa utoaji wa noti za kwanza mwaka 1966, zenye sura ya Mwalimu Julius Nyerere na picha ya Mlima Kilimanjaro, ulikuwa ishara ya kujitegemea kwa taifa na uwezo wake wa kujenga mustakabali wake wa kiuchumi.
Aidha, alieleza kuwa kwa sasa majukumu ya Benki Kuu yamepanuka zaidi na kugusa maisha ya kila siku ya wananchi, wakiwemo walimu, wafanyabiashara wadogo na vijana wajasiriamali, ambao wanategemea uthabiti wa sekta ya fedha katika kufanikisha malengo yao.
Katika hatua nyingine, alipongeza Mpango wa Ununuzi wa Dhahabu ya Ndani ulioanzishwa mwaka 2024, ambao umeiwezesha Benki Kuu kununua zaidi ya tani 25 za dhahabu hadi kufikia Mei 2026, na hivyo kuimarisha akiba ya fedha za kigeni.
Kwa upande wake, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, alisema kuwa katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, uchumi wa Tanzania umekua kwa wastani wa asilimia 6.2, kiwango kinachozidi wastani wa asilimia 4.4 kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Aliongeza kuwa mfumuko wa bei umeendelea kudhibitiwa katika kiwango cha tarakimu moja, ukiwa na wastani wa asilimia 7.5 katika kipindi hicho.
Hata hivyo, katika miaka mitatu iliyopita, hali imeimarika zaidi ambapo wastani wa mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.5, ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia 3 hadi 5.Bw. Tutuba alibainisha kuwa mafanikio hayo ni makubwa ikilinganishwa na kiwango cha juu cha mfumuko wa bei cha asilimia 35.3 kilichorekodiwa mwaka 1994, akisisitiza kuwa hatua zilizochukuliwa zimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha uthabiti wa uchumi wa nchi.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa kitaifa na kimataifa, wakiwemo Magavana wa Benki Kuu kutoka EAC na SADC.







