DCEA yakamata kilo milioni sita za dawa za kulevya katika miaka mitatu ya Kamishna Jenerali Aretas James Lyimo

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas James Lyimo amesema,mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama imefanikiwa kukamata zaidi ya kilogramu milioni sita za dawa za kulevya za aina mbalimbali tangu alipoteuliwa kuongoza taasisi hiyo mwaka 2023.
Ameyabainisha hayo Juni 24,2026 wakati wa mahojiano maalum na Clouds TV jijini Dar es Salaam ambapo mafanikio hayo ni matokeo ya operesheni endelevu zinazofanywa mchana na usiku kwa lengo la kuzuia kuingia, kusambazwa na kutumiwa kwa dawa za kulevya nchini.

“Tangu niteuliwe mwaka 2023 hadi sasa, kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama, tumefanikiwa kukamata zaidi ya kilogramu milioni sita za dawa za kulevya. Hii ni idadi kubwa sana ambayo inaonesha ukubwa wa tatizo,lakini pia mafanikio ya juhudi zinazofanyika katika mapambano haya."

Amesema,maafisa wa DCEA na vyombo vingine wanaendelea kufanya kazi muda wote ili kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanalindwa dhidi ya athari za dawa za kulevya ambazo ni tishio kwa maendeleo na usalama wa taifa.

Kwa mujibu wa Lyimo, uchunguzi uliofanywa na mamlaka hiyo umebaini kuwa kundi kubwa la waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya ni vijana, hususan wanafunzi wa vyuo vikuu, ambao mara nyingi huanza kutumia dawa hizo bila kutambua madhara yake na baadaye kujikuta katika uraibu mkubwa.

Amesema,matumizi ya dawa za kulevya ni changamoto ya kimataifa inayohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, ikiwemo serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za elimu, wazazi na jamii kwa ujumla ili kuzuia kizazi cha vijana kuendelea kuathirika.

Kamishna Jenerali Lyimo amebainisha kuwa, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kudhibiti usambazaji wa dawa za kulevya aina ya Cocaine, Heroin, Mandrax na Methamphetamine ambazo hapo awali zilikuwa zikitumika kwa kiwango kikubwa na kuathiri maisha ya vijana wengi.

Amesema,mafanikio hayo yameifanya Tanzania kutambuliwa kimataifa, huku baadhi ya mataifa yakionesha nia ya kujifunza mbinu zinazotumiwa na DCEA katika kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya.

“Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza upatikanaji wa dawa hizo nchini kutokana na mikakati madhubuti tuliyoiweka pamoja na ushirikiano wa karibu na vyombo vingine vya dola. Lengo letu ni kulinda nguvu kazi ya taifa ambayo kwa kiasi kikubwa inaundwa na vijana."

Pia, Kamishna Jenerali Lyimo amekumbusha kuwa,miaka ya nyuma Tanzania ilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyotumika kama njia kuu ya kupitisha dawa za kulevya kwenda mataifa mengine kutokana na nafasi yake ya kijiografia na uwepo wa ukanda mrefu wa pwani.
Amesema,wafanyabiashara wa dawa za kulevya walikuwa wakitumia majahazi kutoka baadhi ya mataifa ya Asia kuingiza dawa hizo nchini kabla ya kusambazwa katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Hata hivyo, amesema kuimarishwa kwa doria, mifumo ya ufuatiliaji na ushirikiano wa kimataifa kumechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza njia hizo za usafirishaji.

Aidha, Kamishna Jenerali Lyimo ameonya kuhusu ongezeko la matumizi ya kemikali bashirifu katika utengenezaji wa dawa za kulevya za kisasa, akisema changamoto hiyo imeibuka kutokana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kubadili mbinu baada ya njia za kawaida za usafirishaji kudhibitiwa.

Amefafanua kuwa,kemikali bashirifu ni kemikali halali zinazotumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile viwandani, katika sekta ya madini, hospitali, maabara za shule na katika uzalishaji wa dawa.

Hata hivyo, amesema baadhi ya wahalifu wamekuwa wakizitumia vibaya kemikali hizo kutengeneza dawa za kulevya ambazo ni hatari zaidi kwa afya ya binadamu.

“Kadri teknolojia inavyokua na usafirishaji wa dawa za kulevya kuwa mgumu zaidi, baadhi ya wahalifu wamehamia katika utengenezaji wa dawa hizo kwa kutumia kemikali bashirifu. Hili ni tishio kubwa kwa sababu dawa zinazozalishwa kwa njia hiyo zina madhara makubwa sana kwa watumiaji."

Ameeleza kuwa,dawa zinazotengenezwa kwa kutumia kemikali bashirifu huathiri kwa haraka mfumo wa fahamu na ubongo, na mara nyingi husababisha utegemezi mkubwa kwa mtumiaji kiasi cha kushindwa kuendesha maisha yake ya kawaida bila kutumia dawa hizo.

Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali Lyimo, Serikali imeendelea kuimarisha udhibiti wa kemikali bashirifu ili kuzuia kuingia kwake nchini bila kufuata taratibu na kuhakikisha haziishii mikononi mwa watu wenye nia ovu.

Vilevile amesema,matumizi ya teknolojia yamekuwa silaha muhimu katika vita dhidi ya dawa za kulevya, kwani yameongeza uwezo wa mamlaka kubaini na kufuatilia mitandao ya wahalifu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.
Amesema,mifumo ya kidijitali na uchambuzi wa taarifa za kielektroniki umewezesha kubaini wahusika wa matukio mbalimbali ya uingizaji wa dawa za kulevya nchini, ikiwemo baadhi ya operesheni zilizofanikiwa kukamata mizigo ya dawa za kulevya katika maeneo ya bandari na mipaka ya nchi.

“Teknolojia imetupa uwezo mkubwa wa kufuatilia mienendo ya wahalifu na kubaini mitandao yao. Leo hii tunaweza kugundua wahusika hata pale wanapotumia njia za kidijitali kufanya mawasiliano au kuagiza mizigo yao kwa siri."

Amesisitiza kuwa,DCEA itaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia, ushirikiano wa kimataifa na operesheni za pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha Tanzania inabaki salama dhidi ya tishio la dawa za kulevya na kulinda mustakabali wa vijana wa taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here