Jaji Mkuu amshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuendelea kuimarisha Mahakama

Asema Rais Samia anasimamia kwa dhati kauli yake ya kuitaka Mahakama ya Tanzania kuwa Mhimili wenye hadhi Duniani

■ Amshukuru pia kwa Uteuzi wa Mtendaji Mkuu mpya

· Awataka watumishi wote wa Mahakama kumpa ushirikiano Mtendaji huyo

■ Ampongeza Prof. Ole Gabriel kwa kazi nzuri na kustaafu kwa heshima

■ Awakumbusha watumishi wa Mahakama kuzingatia Utii na Bidii katika Utumishi

NA MARY GWERA
Mahakama

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendelea kuuimarisha Mhimili wa Mahakama nchini kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo uteuzi wa Majaji, ongezeko la bajeti na masuala mengine.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kushoto) akimkaribisha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kushoto) akimuaga na kumtakia kila la kheri Mtendaji Mkuu mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (kushoto) na Mtendaji Mkuu mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) mara baada ya Kikao maalum cha Jaji Mkuu na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha Kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. Jingu na kumuaga Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama, Prof. Ole Gabriel tarehe 24 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

Mhe. Masaju aliyasema haya jana tarehe 24 Juni, 2026 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu, Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma wakati wa kikao maalum kati yake na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha Kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Antony Jingu na kumuaga kwa heshima Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel.

“Sisi tuna wajibu wa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa nia yake ya dhati kabisa ya kuona kwamba Mhimili huu unatekeleza wajibu wake wa kutoa haki kwa ufanisi ipasavyo ili kusogeza mbele ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa,” alisema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amesema kuwa, Rais Mhe. Dkt. Samia anaendelea kuiishi kauli yake ya kuiwezesha Mahakama ili kuhakikisha Mhimili huo unakuwa moja kati ya Mihimili yenye hadhi duniani kauli jambo ambalo alimuelekeza Jaji Mkuu kulisimamia alipomuapisha tarehe 15 Juni, 2025 na vilevile kulisisitiza alipomuapisha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama tarehe 19 Juni, 2026.

Ameongeza, kwa kumshukuru Mhe. Dkt. Samia kwa kuendelea kuongeza bajeti ya Mahakama hata katika mazingira magumu, kuendelea kuiwezesha Mahakama kwenye rasilimaliwatu, vitendea kazi.

“Mwaka uliopita, tumeona na tumeshuhudia kwa mfano ukiacha majengo ambayo ni kitendea kazi kikubwa sana, magari, uteuzi wa Majaji, ongezeko la nafasi za ajira, Huduma ya Bima ya Afya kwa Watumishi mambo ambayo yanaongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi,” amesema.

“Namshukuru pia Mhe. Rais kwa kumteua Dkt. Jingu kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Dkt. Jingu wewe unakuwa wa nne, namba nne ina maana kubwa sana kiroho, bahati ndio unarithi kwa Mtendaji Mkuu Mstaafu ambaye amefanya vizuri ambaye mmekuwa na mahusiano mazuri, anakurithisha na timu nzuri hii ya Menejimenti tuna kila sababu ya kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwangu mimi ni faraja kubwa sana kwamba Mhe. Rais alikuona ndio maana namshukuru kwa kukuteua,” amesisitiza Mhe. Masaju.

Jaji Mkuu ameeleza kuwa, “kadri unavyokuwa na madaraka makubwa ndivyo unavyozidi kuwa tegemezi kwa watu wengine zaidi na kwa kadri hiyo hiyo ndivyo unavyopasawa kuwa mnyenyekevu ili hao unaowategemea wakufanyie kazi zao wakufikie na wewe wakufikie ujue changamoto zao ili wakusaidie ili muende.”

Ameongeza kuwa, “kadri unavyokuwa na madaraka makubwa ni kwa kiwango hicho hicho unazidi kuwa mtumishi wa wote. Sasa ndugu yangu huu utumishi umehamia kwako, sasa wewe ni mtumishi wa wote sisi tunakutegemea yaani mpaka yule Hakimu aliyepo Mahakama ya Mwanzo na Mhudumu wake na Karani wake wote wanakutegemea wewe.”

Aidha, Jaji Mkuu amemtaka Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama kuendeleza ushirikiano na mahusiano mazuri na wadau wa Mahakama sambamba na kuendeleza yote mazuri aliyoacha mtangulizi wake Prof. Ole Gabriel pamoja na kuwa mbunifu kwa kuanzisha mambo mengine zaidi ili kuhakikisha kwamba mipango iliyopo inatekelezwa kwa ufanisi ipasavyo.

Vilevile, Mhe. Masaju amemtaka Dkt. Jingu kuendeleza na kumaliza miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama nchini ili wananchi waweze huduma ya haki. Ametoa mifano ya majengo yanayotakiwa kumalizika mwaka huu ikiwa ni pamoja na majengo ya Mahakama za Wilaya Mkalama na Chamwino na mengine ili kuwaondolea shida wanayopata wananchi wa maeneo hayo kufuata huduma ya haki mbali.

Kadhalika, katika kikao hicho, Mhe. Masaju amekumbusha mambo muhimu ya kuzingatia katika utumishi wa umma ambayo ni pamoja na bidii ya kazi na utii kwa mamlaka.

“Mtumishi lazima awe na bidii ya kazi, lakini mtumishi lazima awe mtii maana asipokuwa mtii huyo hawezi tena kuwa mtumishi, na kosa kubwa sana katika utumishi wa umma ‘Insurbodination’ kudharau/kutotii mamlaka,” amesisitiza Mhe. Masaju huku akiwataka wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania na watumishi wa kumtii na kumpa ushirikiano Mtendaji Mkuu mpya.

Aidha, Jaji Mkuu amesema, Utii unabeba mambo mengi ambayo ni pamoja na kutii Katiba na Sheria za Nchi kama inavyotajwa katika Ibara ya 26 na kutii masuala yote yanayohusu maadili ya Taasisi unayofanyia kazi, kutii maelekezo yoyote ambayo ni halali, na kwamba mtumishi akiweza kuzingatia hayo ndio umuhimu wake unazidi kuonekana.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza wakati wa wakati wa Kikao maalum kati yake na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha Kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Antony Jingu na kumuaga Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel tarehe 24 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Kadhalika, Mhe. Masaju amezungumzia kuhusu suala la kuendelea kuimarisha ushirikiano na mahusiano na wadau wengine Serikalini na Bunge.

Katika hatua nyingine Mhe. Masaju amemdokeza Mtendaji Mkuu, Dkt. Jingu juu ya Kaulimbiu ya Mahakama ya mwaka 2026; ‘Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa.’ 

Amesema, “Mimi mara nyingi natembeaga na Dira ya Taifa ya Maendeleo, ukiangalia ule msingi mkuu wa Dira, akaangalia na vile vipaumbele vyake vinne, ukaangalie na zile nguzo tatu unakuta yote yale ni masuala ya Utawala wa Sheria, ili twende tufikie hiyo hatua tunayotaka lazima tuziishi sheria kwa sababu kila kitu kinasimamiwa na kutawaliwa na sheria.”

“Zipo sheria sasa hivi ninafanya kazi hapa, nina kila kipengele kilichoainishwa pale na sheria zake, unapoenda nguzo ya tatu Tabia Nchi na Mazingira tayari tunaainisha Sheria zinazohusika, lakini Katiba ikiwa kila sehemu, unapoenda Nguzo ya Pili ‘Human Capacity and Development’ ile ina sheria zake, unapoenda nguzo ya kwanza ya Uchumi nayo ina sheria zake,” ameeleza Jaji Mkuu.

Ameongeza kuwa, katika Vipaumbele na Msingi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 vinazungumza juu ya Utawala, Usalama, Amani, Utulivu. Amesema, ni vema kusimamia na kutekeleza ipasavyo sheria mbalimbali ambazo zinaendana na vipaumbele vya Dira hiyo ambavyo ni Utawala Bora na Haki, Serikali za Mitaa Imara zinazowajibika, Utumishi wa Umma Unaowajibika na Amani, Usalama na Utulivu.

“Zipo sheria zinazosimamia masuala hayo, mfano zipo Sheria zinazosimamia Amani, Usalama na Utulivu ambazo ni pamoja na Sheria za Polisi, Sheria za Usalama, Sheria za Madawa ya Kulevya, na kadhalika. Na kwa namna hiyo Taifa ndipo linapoweza kustawi na likawa na maendeleo,” amesema Mhe. Masaju na kumpongeza Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama kwa kuonesha kuielewa vizuri Dira hiyo sambamba na kuelewa maelekezo ya Rais Samia ya kutaka Mhimili wa Mahakama ya Tanzania uwe moja ya Mihimili yenye hadhi Duniani.
Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju alipokuwa akitoa neno wakati wa Kikao maalum kati yake na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha Kumkaribisha rasmi Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Antony Jingu na kumuaga Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel tarehe 24 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu yaWajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania. Kushoto ni Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (kushoto) na kulia Mtendaji Mkuu mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.(Picha na MARY GWERA, Mahakama).

Amesema zipo sheria mbalimbali zinazosimamia masuala mbalimbali, mfano sheria za kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara na nyingine nyingi.

Aidha, katika hotuba yake Jaji Mkuu amempongeza Mtendaji Mkuu Mstaafu kwa Taarifa ya Makabidhiano iliyoandaliwa kwa kina na kuelekeza kuwa, taarifa hiyo ambayo ipo kwenye kitabu isambazwe katika Mahakama zote nchini ili itumike kama kitendea kazi katika utekelezaji wa shughuli za Mahakama.

“Nimshukuru Mhe. Rais, moja kwa kukuteua katika nafasi mbalimbali na mpaka sasa kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, kazi ambayo umeifanya kwa ufanisi mkubwa sana ukiwa umerithi kwa Watangulizi wako, umemsema Mhe. Balozi Hussein Kattanga na Ndugu Mathias Kabunduguru. Sasa umefanya vizuri kwa ufanisi mkubwa sana, mwaka mmoja ambao tumefanya kazi wote hapa, kuna mambo makubwa sana ambayo yamefanyika,” amesema Jaji Mkuu.

“Nimeona hii taarifa nzuri uliyoandaa, sisi kama Viongozi ndivyo tunavyopaswa kufanya, tunarithishana kwa namna hii, hii nyaraka kwanza inasomeka kirahisi na inafaa kwa matumizi, hii ni nyaraka ya kudumu na ina maana kubwa sana. Sasa taarifa haikumaanisha iwe kati ya Prof. Ole Gabriel na Dkt. Jingu bali taarifa hii inatuhusu sisi sote, sisi Menejimenti tukiwa injini ya uongozi wa Mahakama ya Tanzania, hii inamuhusu kila mmoja wetu, kwahiyo mlizingatie tulifanyie kazi,” amesisitiza.

Mhe. Masaju amempongeza Prof. Ole Gabriel kwa alichokifanya na kusema kwamba, utumishi wa umma ndivyo unapaswa kuwa hivyo kutokuoneana wivu, kutokuhujumiana, kutokuoneana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here