Profesa ole Gabriel amshukuru Rais Dkt.Samia kwa kumpa nafasi ya kuitumikia Mahakama miaka mitano iliyopita

NA JAMES BUSANYA, 
Mahakama-Dodoma

MTENDAJI Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kulitumikia Taifa kupitia nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama miaka mitano iliyopita.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kushoto) akimuaga na kumtakia kila la kheri Prof. Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania.(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma).

Prof. Ole Gabriel aliyasema hayo jana tarehe 24 Juni, 2026 Makao Makuu ya Mahakama Jijini Dodoma wakati wa Kikao maalum cha Jaji Mkuu na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha kumkaribisha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Antony Jingu na kumuaga Mtendaji Mkuu huyo aliyestaafu.

Alisema kuwa, uteuzi wake ni tukio ambalo hataweza kulisahau katika maisha yake kwa kuwa Rais alimuona kuwa miongoni mwa Watanzania waliostahili kupewa dhamana ya kuiongoza Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kipindi hicho.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu katika kipindi chote cha utumishi wangu Serikalini na Mahakamani,” alisema.

Aidha, amewashukuru Viongozi na Wajumbe wote wa Menejimenti ya Mahakama kwa ushirikiano, ushauri na kujitolea kwao, akisema mchango wao umewezesha kupatikana kwa mafanikio mbalimbali katika kipindi chake cha utumishi. Ameishukuru pia familia yake hususan mkewe Bi. Devotha kwa ushirikiano aliompatia wakati wa utumishi wake.

Kwa namna ya pekee, alimshukuru Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoja na aliyekuwa Jaji Kiongozi ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Eliezer Mbuki Feleshi, ambapo amesema alipojiunga na Mahakama, walimpokea vizuri na kumpatia maarifa na uzoefu uliomuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Pia alimpongeza mke, Bi. Devotha wake kwa uvumilivu, msaada na mchango mkubwa alioutoa katika kipindi chote cha utumishi wake.
Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa neno wakati wa Kikao maalum cha Jaji Mkuu na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania cha kumkaribisha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Antony Jingu na kumuaga Mtendaji Mkuu huyo aliyestaafu. Kikao hicho kilifanyika jana tarehe 24 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
"Mhe. Jaji Mkuu, ingawa tumefanya kazi pamoja Mahakamani kwa kipindi cha mwaka mmoja, lakini tumefahamiana kwa muda mrefu zaidi kabla sijaja Mahakamani. Ushauri na mchango wako katika masuala ya kisheria ulinisaidia sana hata kipindi nilipokuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo,” ameeleza Prof. Ole Gabriel.

Amebainisha kwamba, mafanikio yaliyopatikana Mahakamani yamejengwa katika misingi ya ushirikiano mzuri kati ya Ofisi ya Jaji Mkuu, Ofisi ya Jaji Kiongozi, Ofisi ya Msajili Mkuu wa Mahakama, Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama pamoja na Menejimenti nzima ya Mahakama.

Alisisitiza kuwa, ushirikiano na kuheshimiana kati ya Maofisa wa Kada za Mahakama na wale wasio wa kada hizo umekuwa msingi muhimu wa mafanikio ya Taasisi hiyo.

Katika hatua nyingine, Prof. Ole Gabriel amempongeza Dkt. Jingu kwa kuteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, huku akimshauri kutekeleza majukumu yake kwa bidii, uadilifu na weledi.

Alisema kazi hiyo ni kubwa na yenye matarajio makubwa kutoka kwa Watanzania, licha ya kuonekana ya kawaida kwa mtazamo wa nje lakini ukiingia ndani utaona uhalisia.

“Taasisi hii ina wataalamu wazuri, mazingira bora ya kazi na watu wenye utayari wa kushirikiana. Usitishike, fanya kazi kwa bidii na pale utakapohitaji ushauri sisi tuliokutangulia tutakuwa tayari kukusaidia,” amesema.
Sehemu ya wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakimsikiliza Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alipokuwa akitoa neno wakati wa Kikao maalum kilichoandaliwa kwa ajili ya kumkaribirsha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Anthony Jingu na Kumuaga, Prof. Ole Gabriel ambaye amestaafu. Kikao hicho kilifanyika jana tarehe 24 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel jana tarehe 24 Juni, 2026 wakati wa Kikao maalum kilichoandaliwa kwa ajili ya kumkaribirsha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Anthony Jingu na Kumuaga, Prof. Ole Gabriel ambaye amestaafu.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (kushoto) na Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) wakati wa Kikao maalum kilichofanyika jana tarehe 24 Juni, 2026 kwa ajili ya kumkaribirsha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Dkt. John Anthony Jingu na Kumuaga, Prof. Ole Gabriel ambaye amestaafu.

Ameeleza kuwa, ana imani na uwezo wa Dkt. Jingu kutokana na umahiri wake katika kazi na kujituma kwake, akiongeza kuwa ataendelea kufuatilia maendeleo ya Mahakama hata baada ya kustaafu na kusema kuwa Mahakama ikipiga hatua atafurahi na ikikumbana na changamoto ataguswa kwa sababu amekuwa sehemu ya Taasisi hiyo muhimu.

Akihitimisha hotuba yake, Mtendaji Mkuu huyo mstaafu amemshukuru Jaji Mkuu, Mhe. George Masaju, Viongozi, Menejimenti na Watumishi wote wa Mahakama kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chote cha utumishi wake.

Kadhalika amesema kuwa, ataendelea kuwa tayari kutoa ushauri, msaada na ushirikiano kwa Mahakama na watumishi wake wakati wowote atakapohitajika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here