NA DIRAMAKINI
KOCHA wa timu ya taifa ya Iran, Amir Ghalenoei ameibua tuhuma kubwa dhidi ya waandaaji wa Kombe la Dunia 2026 baada ya kudai kuwa,kikosi chake kililazimishwa kuondoka nchini Marekani na kurejea katika kambi yake ya mazoezi mjini Tijuana, Mexico.
Ni saa chache tu baada ya kumaliza mchezo wake wa kwanza wa michuano hiyo dhidi ya New Zealand.
Iran ilifungua kampeni yake ya Kombe la Dunia kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya New Zealand katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa SoFi (Los Angeles Stadium) uliopo karibu na Jiji la Los Angeles.
Hata hivyo, furaha ya matokeo hayo ilififishwa na kile ambacho viongozi wa timu hiyo wamekiita kuwa ni mazingira magumu ya kiutawala na kidiplomasia yanayoikabili timu hiyo tangu kuanza kwa mashindano.
Akizungumza baada ya mechi, Ghalenoei amesema,timu yake ilitarajia kulala usiku mmoja nchini Marekani ili kuwapa wachezaji muda wa kutosha wa kurejesha nguvu baada ya mchezo huo, lakini walipokea maelekezo ya kuondoka mara moja na kurejea Mexico.
“Hatukupata hata muda wa kupona baada ya mechi. Baada ya mchezo tuliambiwa lazima tuondoke mara moja. Kwa timu ya kiwango hiki, muda wa kupona ni jambo muhimu sana, lakini tulilazimika kupanda ndege na kurejea Tijuana,” alidai kocha huyo kupitia mkalimani.
Ingawa hakutaja ni mamlaka gani iliyotoa agizo hilo, Ghalenoei alieleza kushangazwa na uamuzi huo akidai kuwa ulikiuka ratiba ya awali iliyokuwa imekubaliwa.
“Hatuelewi sababu ya kulazimishwa kurejea. Tulitarajia kufika siku mbili kabla ya mechi na kubaki hadi kesho mchana kabla ya kurudi kambini. Inaonekana kuna watu wengine wanaopanga mambo kwa niaba yetu. Hii ni hali ya kushangaza sana,”amedai.
Malalamiko hayo yanakuja wakati Iran ikiendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zilizochangiwa na mvutano wa kisiasa unaoendelea kati ya Iran kwa upande mmoja na Marekani pamoja na Israel kwa upande mwingine.
Kwa mujibu wa viongozi wa timu hiyo, maandalizi yao ya Kombe la Dunia yameathiriwa kwa kiasi kikubwa tangu kuzuka kwa mzozo huo, huku baadhi ya maofisa muhimu wa Shirikisho la Soka la Iran wakishindwa kuingia Marekani baada ya kunyimwa visa.
Nahodha wa Iran, Mehdi Taremi amesema, safari ya kutoka Tijuana hadi eneo la Los Angeles ambayo kwa kawaida ni fupi, ilichukua takribani saa tano kutokana na ukaguzi mkali wa kiusalama na taratibu mbalimbali za uhamiaji.
“Tunalazimika kuondoka Los Angeles sasa hivi na hali hii si nzuri kwa timu yetu. Nafikiri FIFA inapaswa kutusaidia zaidi. Kwa kweli kila kitu kinaonekana kama janga kwetu,"amesema Taremi.
Pia,Kocha huyo pia alieleza kuwa,baadhi ya wachezaji wake walipata maumivu ya misuli (cramps) wakati wa mchezo kutokana na uchovu uliosababishwa na safari ndefu na maandalizi yasiyokuwa ya kawaida.
“Kabla ya mechi nilisema wazi kwamba hatukupata muda wa kutosha wa kuzoea mazingira kutokana na safari. Wachezaji kadhaa walipata matatizo ya misuli na ndiyo sababu tulifanya mabadiliko. Hayakuwa maamuzi ya kiufundi bali yalitokana na majeraha na uchovu."
Licha ya changamoto hizo, maelfu ya mashabiki wa Iran waliunda mazingira ya kuvutia ndani ya Uwanja wa SoFi, ulioko katika eneo lenye moja ya jamii kubwa zaidi ya Waajemi wanaoishi nje ya Iran.
Mechi hiyo ilifanyika katika mazingira yenye hisia kali za kisiasa. Wakati mamia ya Waajemi wanaoishi Marekani wakifanya maandamano nje ya uwanja wakipinga serikali ya Iran, mashabiki wengi waliokuwa ndani ya uwanja walionesha kuunga mkono timu ya taifa.
Baadhi yao waligeuka na kuupa mgongo uwanja wakati wimbo wa taifa wa Iran ukipigwa, huku wengine wakipeperusha bendera zenye nembo ya “Lion and Sun”, ishara iliyokuwa sehemu ya bendera rasmi ya Iran kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.
Hata hivyo, baada ya mchezo kuanza, mashabiki wengi waliweka tofauti zao za kisiasa pembeni na kuishangilia kwa nguvu timu yao.
“Ilikuwa kama tunacheza nyumbani. Mashabiki walitengeneza mazingira ya ajabu kwa dakika zote 90 za mchezo,”amesema Taremi.
Ndani ya uwanja, New Zealand ilionekana kuwa karibu kupata ushindi baada ya mshambuliaji Elijah Just kufunga mabao mawili katika vipindi tofauti vya mchezo.
Hata hivyo, Iran ilionesha moyo wa kupambana na kufanikiwa kusawazisha mara mbili kupitia mabao ya kuvutia yaliyofungwa na Ramin Rezaeian pamoja na Mohammad Mohebi.
Bao la kusawazisha la Mohebi katika dakika ya 64 lilizua shamrashamra kubwa miongoni mwa mashabiki wa Iran, huku mchezaji huyo akifanya shangwe mbalimbali zilizozua mijadala kwenye mitandao ya kijamii.
Baada ya filimbi ya mwisho, wachezaji wa timu zote walionekana wakikumbatiana na kubadilishana jezi, ishara ya mshikamano licha ya mazingira yenye mvutano yaliyozunguka mchezo huo.
Sare hiyo imeziacha Iran,Ubelgiji,Misri na New Zealand zikiwa na pointi moja kila moja katika kundi lao baada ya mechi za kwanza.
Iran sasa inajiandaa kwa mechi ngumu zaidi dhidi ya Ubelgiji kabla ya kumalizia hatua ya makundi kwa kukutana na Misri, michezo ambayo itaamua hatima ya ndoto zao za kufuzu hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika historia ya ushiriki wao wa Kombe la Dunia.
Pamoja na changamoto zote zinazowakabili, Ghalenoei amesema timu yake haitakata tamaa.
“Tunakabiliwa na vikwazo vingi zaidi kuliko timu nyingine, lakini hatutaruhusu hali hiyo ituzuie kufanya kila tuwezalo. Ninaamini huu ulikuwa mmoja wa michezo bora zaidi ya Kombe la Dunia hadi sasa, na mashabiki walifurahia sana."
