NA DIRAMAKINI
WAKATI mashabiki wengi wa soka duniani huondoka viwanjani mara tu baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, mashabiki wa Timu ya Taifa ya Japan wameendelea kuandika historia tofauti kwa kuonesha kiwango cha juu cha nidhamu na uwajibikaji kinachovutia dunia katika mashindano makubwa ya kimataifa.

Mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Kombe la Dunia la FIFA 2026 kati ya Japan na Uholanzi uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, mamia ya mashabiki wa Japan walibaki katika majukwaa ya Uwanja wa AT&T uliopo Texas, Marekani, wakifanya kile ambacho sasa kimekuwa utambulisho wao katika mashindano ya soka duniani kwa kusafisha maeneo waliyokuwa wamekaa kabla ya kuondoka.
Mashabiki hao walionekana wakikusanya chupa za plastiki, makaratasi,mifuko na taka nyingine zilizokuwa zimetawanyika kwenye sehemu mbalimbali za majukwaa, huku kila mmoja akiwa amebeba mfuko maalumu wa kuhifadhia taka.
Vitendo hivyo vilinaswa na kamera za waandishi wa habari pamoja na mashabiki wengine na kusambazwa kwa kasi katika mitandao ya kijamii, ambapo picha na video zimepokea maelfu ya pongezi kutoka kwa watu wa mataifa mbalimbali waliovutiwa na kiwango hicho cha uwajibikaji.
Wengi wameeleza kuwa,kitendo hicho kinaonesha kuwa ushabiki wa soka unaweza kwenda sambamba na kuheshimu mazingira na mali za umma, jambo ambalo bado ni changamoto katika sehemu nyingi duniani.
Utamaduni huo wa mashabiki wa Japan si jambo jipya. Tangu taifa hilo lianze kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 1998, mashabiki wake wamekuwa wakitambulika kwa tabia ya kusafisha viwanja baada ya mechi, bila kujali kama timu yao imeshinda, imefungwa au imetoka sare.
Kwa miaka mingi, dunia imekuwa ikishuhudia mashabiki hao wakibaki viwanjani kwa muda baada ya mechi kumalizika wakihakikisha maeneo yao yanakuwa safi kabla ya kuondoka, hali inayowafanya kuwa mfano wa kuigwa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Wachambuzi wa masuala ya utamaduni na michezo wanaeleza kuwa tabia hiyo inatokana na misingi ya malezi na elimu inayotolewa nchini Japan, ambapo watoto hujengewa maadili ya kujali mazingira, kuwajibika kwa mali za umma na kushiriki shughuli za usafi tangu wakiwa shuleni.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, falsafa ya jamii ya Japan inahimiza mtu kuwajibika kwa mazingira yanayomzunguka badala ya kusubiri mtu mwingine afanye kazi hiyo, jambo ambalo limejenga kizazi chenye nidhamu na heshima kwa maeneo ya umma.Katika mashindano ya Kombe la Dunia yaliyopita, mashabiki wa Japan waliwahi kusifiwa duniani baada ya kusafisha majukwaa hata katika mechi ambazo timu yao ilipoteza.
Pia,kitendo hicho kilitafsiriwa kama ishara ya ustaarabu na kuheshimu waandaaji wa mashindano pamoja na mashabiki wengine.
Katika Kombe la Dunia 2026, mashabiki hao wameendelea kudumisha sifa hiyo, huku picha zao za kufanya usafi baada ya mechi dhidi ya Uholanzi zikienea duniani na kuzua mjadala chanya kuhusu umuhimu wa kuwajibika kwa mazingira.
Wadau wa michezo wameeleza kuwa,pamoja na ushindani unaoendelea ndani ya uwanja, vitendo vya mashabiki wa Japan vinaonesha kuwa michezo inaweza pia kuwa jukwaa la kufundisha maadili mema, uwajibikaji wa kijamii na utunzaji wa mazingira.
Kadiri mashindano ya Kombe la Dunia yanavyoendelea, mashabiki wa Japan wameendelea kuthibitisha kuwa hawatambuliki tu kwa mapenzi yao kwa soka, bali pia kwa utamaduni wa nidhamu,usafi na heshima unaoifanya dunia kuendelea kuwapongeza na kuwaona kama mfano bora wa kuigwa katika michezo ya kimataifa.