NA DIRAMAKINI
MABINGWA mara mbili wa Kombe la Dunia, timu ya taifa ya Uruguay imelazimika kufanya kazi ya ziada kujiokoa dhidi ya Saudi Arabia.
Ni baada ya kutoka nyuma kwa bao moja na kulazimisha sare ya 1-1 katika mchezo wa Kundi H uliopigwa kwenye dimba la Miami, Florida nchini Marekani.
Matokeo hayo yameifanya Uruguay kushindwa kuonesha makali yake mbele ya wapinzani hao wa Mashariki ya Kati, huku Saudi Arabia ikionesha nidhamu kubwa ya ulinzi na uwezo wa kuhimili mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa Wauruguay.
Saudi Arabia ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Abdulelah Al Amri dakika ya 41, bao lililowapa morali kubwa na kuwafanya kwenda mapumzikoni wakiwa mbele kwa mabao 1-0.
Uruguay ilirejea kipindi cha pili ikiwa na dhamira ya kutafuta angalau pointi moja na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 80 baada ya Maximiliano Araujo kufunga bao la kusawazisha.
Sare hiyo ni ya pili mfululizo katika Kundi H baada ya mchezo mwingine wa kundi hilo kumalizika kwa sare tasa kati ya Hispania na Cape Verde, hali inayofanya ushindani wa kufuzu hatua inayofuata kuwa mkali zaidi huku hakuna timu iliyofanikiwa kujitenga kileleni mwa kundi hilo.
Kwa upande mwingine, katika mchezo wa Kundi G uliochezwa katika dimba la Los Angeles, Inglewood, California, timu ya taifa ya Iran nayo ilijikuta ikikwama baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya New Zealand.
New Zealand ilianza mchezo kwa kasi na kufungua ukurasa wa mabao mapema dakika ya saba kupitia mshambuliaji Elijah Henry Just, aliyewapa timu yake mwanzo mzuri.
Hata hivyo, Iran ilisawazisha dakika ya 32 kupitia kwa Ramin Rezaeian, na kufanya timu hizo kwenda mapumzikoni zikiwa zimefungana bao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa New Zealand kurejesha tena uongozi wake baada ya Elijah Just kufunga bao lake la pili katika dakika ya 54 na kuifanya Iran kuwa katika wakati mgumu.
Hata hivyo, Wairan walionesha moyo wa kupambana na kufanikiwa kusawazisha tena kupitia kwa Mohammad Mohebi dakika ya 64, bao lililohakikisha timu hizo zinagawana pointi.
Matokeo hayo yanaifanya New Zealand kuendelea kujivunia kiwango bora ilichoonesha dhidi ya moja ya timu zenye uzoefu mkubwa kutoka bara la Asia, huku Iran ikishindwa kutumia ubora wake wa kiufundi kuondoka na ushindi.
Sare hiyo pia ni ya pili mfululizo katika Kundi G baada ya mchezo mwingine wa kundi hilo kumalizika kwa sare ya mabao 1-1 kati ya Ubelgiji na Misri.
Hali hiyo imeacha kundi hilo likiwa wazi kwa timu zote nne kuendelea kupigania nafasi za kufuzu hatua inayofuata.
Kwa ujumla, matokeo ya michezo ya Kundi G na H yameonesha ushindani mkubwa wa michuano hiyo, ambapo timu zinazopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri zimejikuta zikikwama mbele ya wapinzani waliodhamiria kupata matokeo chanya.
Aidha,kadri michuano inavyoendelea, kila pointi inaonekana kuwa muhimu katika mbio za kufuzu hatua za mtoano.
