NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Kuwait imetangaza mabadiliko makubwa katika sera zake za ajira kwa wafanyakazi wa ndani baada ya kuamua kuruhusu ajira kutoka nchi 10 pekee zilizoidhinishwa, huku ikizuia ajira kutoka nchi nyingine 27 katika hatua inayolenga kuimarisha usimamizi na udhibiti wa sekta hiyo.
Uamuzi huo umetolewa kupitia waraka mpya wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kuwait, ikiwa ni sehemu ya marekebisho ya kanuni na taratibu zinazohusu ajira za wafanyakazi wa majumbani nchini humo.
Serikali imesema,hatua hiyo imechukuliwa baada ya mapendekezo kutoka taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Afya pamoja na Mamlaka ya Umma ya Nguvukazi.
Kwa mujibu wa kanuni hizo mpya, wafanyakazi wa ndani wataendelea kuajiriwa kutoka nchi za Afrika Kusini, Benin, Eritrea, Ethiopia, Ufilipino, Sri Lanka, India, Vietnam na Nepal.
Aidha, Senegal imeorodheshwa miongoni mwa nchi zinazoruhusiwa, lakini kwa masharti kwamba ajira zitahusu wafanyakazi wa kiume pekee.
Mamlaka za Kuwait zimeeleza kuwa,taratibu zote za uajiri zitafanyika kupitia magavana wa mikoa na vituo rasmi vya huduma, hatua inayotarajiwa kuongeza uwazi na ufanisi katika mchakato wa kuingiza wafanyakazi wa ndani nchini humo.
Wakati huo huo, serikali imezuia ajira za wafanyakazi wa ndani kutoka nchi 27, nyingi zikiwa kutoka bara la Afrika.
Nchi hizo ni pamoja na Kenya, Uganda, Nigeria, Togo, Malawi, Chad, Djibouti, Niger, Guinea, Guinea-Bissau, Sierra Leone, Liberia, Mali, Burkina Faso, Gambia, Cameroon, Rwanda, Burundi, Angola, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nyinginezo.
Pia nchi za Madagascar na Bhutan zimejumuishwa katika orodha hiyo ya marufuku.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa,kwa baadhi ya nchi zilizowekewa vikwazo, marufuku hizo zinawahusu wafanyakazi wa kike pekee, huku ajira za wanaume zikiendelea kuruhusiwa kwa masharti maalumu.
Hata hivyo, mamlaka hazijabainisha mara moja nchi ambazo zimeathiriwa na utaratibu huo wa sehemu.
Wachambuzi wa masuala ya ajira wanaona hatua hiyo kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Kuwait wa kudhibiti soko la ajira za ndani, kuimarisha ufuatiliaji wa wafanyakazi wa kigeni na kuhakikisha taratibu za ajira zinaendeshwa kwa kuzingatia viwango vya kisheria na kiutawala.
Uamuzi huo unakuja siku chache baada ya Kuwait kuzindua mfumo mpya wa kidijitali kupitia programu ya serikali ya “Sahel”, unaowezesha wananchi na wakazi wa nchi hiyo kuomba na kusimamia huduma zinazohusiana na wafanyakazi wa ndani na madereva kwa njia ya mtandao.
Serikali imeeleza kuwa hatua hizo zote ni sehemu ya mageuzi yanayolenga kurahisisha huduma za umma na kuimarisha usimamizi wa sekta ya ajira.
Mabadiliko hayo yanatarajiwa kuwa na athari kwa maelfu ya wafanyakazi wanaotegemea soko la ajira la Kuwait, pamoja na nchi zinazotuma wafanyakazi wa ndani katika taifa hilo la Ghuba, ambalo kwa miaka mingi limekuwa moja ya masoko makubwa ya ajira kwa wafanyakazi kutoka Asia na Afrika. (Gulf News)
