Mexico yaifunga Afrika Kusini mabao 2-0 na kuongoza Kundi A ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026

NA DIRAMAKINI

TIMU ya Taifa ya Mexico imeanza vyema kampeni yake ya FIFA World Cup 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya South Africa katika mchezo wa ufunguzi uliochezwa Juni 11, 2026, kwenye Uwanja wa Mexico City Stadium (zamani Estadio Azteca) jijini Mexico City.
Mbele ya maelfu ya mashabiki walioufanya uwanja huo kufurika, wenyeji Mexico walionesha ubora wao tangu dakika za mwanzo za mchezo na kufanikiwa kupata bao la kwanza mapema kupitia mshambuliaji Julián Quiñones katika dakika ya tisa, bao ambalo pia limeingia kwenye historia kama moja ya mabao ya kwanza ya michuano hiyo ya mwaka 2026.

Baada ya bao hilo, Afrika Kusini ilijaribu kurejea mchezoni,lakini ilikumbana na ugumu mkubwa wa kuhimili mashambulizi ya wenyeji ambao walitawala sehemu kubwa ya mchezo.

Safu ya ulinzi ya Bafana Bafana ilionekana kuyumba mara kadhaa huku viungo wa Mexico wakitengeneza nafasi nyingi za kufunga.

Katika kipindi cha pili, Mexico iliendelea kushambulia na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 67 baada ya mshambuliaji mkongwe Raúl Jiménez kufunga bao la pili na kuipa timu yake uongozi wa mabao 2-0.

Bao hilo lilizima matumaini ya Afrika Kusini ya kusaka sare katika mchezo huo muhimu wa ufunguzi.

Matokeo hayo yanaifanya Mexico kujikusanyia alama tatu muhimu za kwanza na kuongoza msimamo wa Kundi A, huku ikiweka msingi mzuri wa kutafuta nafasi ya kufuzu hatua ya mtoano katika mashindano hayo yanayoshirikisha timu 48 kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia.

Kwa upande wa Afrika Kusini, kipigo hicho kinamaanisha italazimika kutafuta matokeo mazuri katika michezo yake ijayo ili kuendelea kuwa na matumaini ya kusonga mbele kwenye mashindano hayo makubwa zaidi ya soka duniani.

Ushindi huo pia umeipa Mexico mwanzo mzuri mbele ya mashabiki wake wa nyumbani katika michuano ambayo kwa pamoja inaandaliwa na Mexico, Marekani na Canada.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here