DODOMA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI, Mhe.Profesa. Riziki Shemdoe (Mb), ameipongeza Wizara ya Fedha kwa kuendelea kutekeleza kwa weledi majukumu yake ikiwemo kuandaa Bajeti ya Serikali iliyokubalika na kupitishwa kwa kishindo na wawakilishi wa wananchi bungeni jijini Dodoma leo Juni 23,2026.
Pongezi hizo amezitoa alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, kabla ya kufunga Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi. Dkt. Moses Kusiluka.
“Kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Mhe. Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar na Wizara yake kwa ujumla, kwa Bajeti Kuu ya Mwaka 2026/2027, leo hii kupita kwa kishindo, tumepiga kura na zaidi ya asilimia tisini na saba, tunamshukuru Mhe. Waziri kwa kuandaa bajeti ambayo imekubalika na wananchi na wawakilishi wa wananchi."
Amesema,Wizara ya Fedha ina jukumu kubwa la kuhakikisha fedha za maendeleo zinapatikana ili kurahisisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili wananchi wapate huduma zote muhimu ikiwemo huduma za afya, miundombinu bora inayowezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo biashara.
‘’Ninawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya kama Wizara ya Fedha, kwa sababu bila nyinyi fedha zisingeweza kushuka kule ambako tupo sisi watekelezaji, hongereni kwa kuwa hapa kwenye Wiki ya Utumishi wa Umma, nina imani mmepata mambo mengi kutoka kwa wananchi na watumishi wenzenu ninawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya,’’ amesema Mhe.Prof.Shemdoe.
Awali, akizungumza na watumishi wa Wizara ya Fedha, katika Banda la Wizara, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Fedha, Bw. Simbani Liganga, amewaagiza watumishi hao kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi mkubwa, katika Maonesho ya Sabasaba yanayotarajiwa kuanza Juni 28, 2026, kama walivyotekeleza majukumu hayo katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, yaliyofanyika jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa, Wizara ya Fedha na taasisi zake, zinatumia maadhimisho na maonesho mbalimbali kama njia muhimu ya kuwafikia wananchi na wadau wake kwa wingi hivyo ni vyema watumishi wa Wizara ya Fedha, kutumia fursa hiyo kueleza wananchi majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Wizara, kuwahudumia wananchi ipasavyo ikiwemo kuwapa elimu katika masuala ya fedha na uwekezaji.
‘’Napenda kutoa wito kwa watumishi wenzangu ambao toka mwanzo wa Maonesho haya wamekuwa wakijitolea kufanya kazi kwa nguvu zote kutoa huduma kwa wananchi, kwa sasa tunaenda Dar es Salaam kwa ajili ya Maonesho ya Sabasaba, nitoe wito kwa watumishi wenzangu kuendelea na ari hii hii ambayo mmeionesha hapa Dodoma,"ameongeza Bw. Liganga.
Amewasihi wananchi kutembelea Wizara ya Fedha, katika Maonesho ya Sabasaba yanayotarajiwa kuanza Juni 28, 2026 mara tu baada ya Maonesho kuanza, ili kupata fursa mbalimbali ikiwemo elimu kuhusu masuala ya fedha, bajeti, uwekezaji pamoja na kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara ya Fedha.
‘’Natoa wito kwa wakazi wa jiji laDar es Salaam na mikoa jirani watembelee Banda la Wizara ya Fedha, ili waweze kupata huduma na wajionee kazi ambazo tunazifanya,"amesema Bw. Ligaga.
Maafisa kutoka Idara na Vitengo mbalimbali vya Wizara ya Fedha, ikiwemo Idara ya Bajeti, Idara ya Pensheni, Idara ya Usimamizi wa Sera za Ununuzi wa Umma, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Hazina SACCOSS, wanatarajia kushiriki na kutoa huduma kwa wananchi na kueleza majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Wizara ya Fedha.
Tags
Chinangali Park Dodoma
Habari
Profesa Riziki Shemdoe
Wiki ya Utumishi wa Umma Tanzania
Wizara ya Fedha Tanzania







