NA GODFREY NNKO
SERIKALI imepokea rasmi mapendekezo ya kimkakati ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini nchini yaliyowasilishwa na Timu ya Wataalamu iliyoundwa kuishauri Wizara ya Madini kuhusu njia bora za kuimarisha uchimbaji mdogo wa madini na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Mapendekezo hayo yamewasilishwa leo Juni 13, 2026 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt.Victor Tesha katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Madini,Mheshimiwa Anthony Mavunde, viongozi wa serikali pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya madini.
Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Profesa Mkumbo amesema,Serikali imejipanga kuyafanyia kazi mapendekezo hayo kwa haraka kutokana na umuhimu wake katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kuongeza ajira na kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi.
Amesema,mapendekezo hayo yamejikita katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya uchimbaji mdogo wa madini, ikiwemo ukosefu wa mitaji, matumizi ya teknolojia duni, pamoja na upungufu wa taarifa sahihi za kijiolojia zinazohitajika katika shughuli za uchimbaji.
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, uwezeshaji wa wachimbaji wadogo ni hatua muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi shindani unaotoa fursa za ajira na ustawi wa wananchi.
Amesema,maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, yameelekeza mipango yote ya maendeleo kujibu changamoto kuu tatu za taifa ambazo ni kuongeza mitaji kwa wananchi, kuzalisha ajira na kupunguza umaskini.
“Tunapowawezesha wachimbaji wadogo kupata mitaji, teknolojia na taarifa sahihi za kijiolojia, tunafungua fursa za kuongeza uzalishaji, kukuza ajira na kuongeza kipato cha wananchi. Hii ndiyo njia sahihi ya kupambana na umaskini kwa kiwango kikubwa."
Amebainisha kuwa,pamoja na ukuaji mkubwa wa uchumi unaoendelea kushuhudiwa nchini, bado kuna umuhimu wa kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanashiriki moja kwa moja katika shughuli za uzalishaji ili waweze kunufaika na matunda ya ukuaji huo.
“Ukuaji wa uchumi lazima uendane na kupungua kwa umaskini na kuongezeka kwa ajira. Hatuwezi kutegemea makampuni makubwa pekee kwa sababu yanatumia teknolojia zinazohitaji watu wachache. Wachimbaji wadogo wana uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira kwa Watanzania wengi."
Katika hatua nyingine, Profesa Mkumbo ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuandaa ripoti hiyo akieleza kuwa,imekuja wakati muafaka ambapo Serikali inaendelea kusukuma ajenda ya kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa madini na kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wengi zaidi.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia kwa uamuzi wa kutenga asilimia 10 ya mapato ya sekta ya madini kwa ajili ya shughuli za utafiti, akisema hatua hiyo ni ya kihistoria na itasaidia kuongeza upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiolojia kwa wachimbaji wadogo.
Ameongeza kuwa,maamuzi yanayozingatia ushahidi wa kisayansi yana nafasi kubwa ya kuleta mafanikio katika sekta mbalimbali za maendeleo, hivyo ripoti hiyo itakuwa nyenzo muhimu katika kufanya maamuzi sahihi kuhusu mustakabali wa sekta ya madini nchini.
Sekta ya Madini yavuka malengo
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde amesema,sekta ya madini imeendelea kuonesha mafanikio makubwa kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato yaliyowekwa na Serikali.
Amesema,hadi Juni 12, 2026 sekta hiyo ilikuwa imechangia zaidi ya shilingi trilioni moja katika Mfuko Mkuu wa Serikali ikiwa ni sehemu ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30, 2026.
Waziri Mavunde amesema,mwaka uliopita sekta hiyo ilikusanya shilingi trilioni 1.3, hali inayodhihirisha mchango mkubwa wa sekta ya madini katika kuimarisha uchumi wa taifa.
Ameeleza kuwa, licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo, kundi hilo linachangia takribani asilimia 40 ya mapato yote ya sekta ya madini, jambo linaloonesha umuhimu wake katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
“Tunao wachimbaji wanaoshindwa kuongeza uzalishaji kutokana na ukosefu wa vifaa muhimu kama pampu na compressor. Ni wakati sasa wa Serikali kuweka mfumo maalumu wa kuwawezesha ili waongeze tija na mchango wao katika uchumi wa taifa."
Waziri Mavunde amebainisha kuwa,Serikali tayari imeanza kutekeleza hatua mbalimbali za kuwawezesha wachimbaji wadogo, ikiwemo kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia mfumo wa dhamana ya mikopo utakaowasaidia kupata mikopo hata wanapokosa dhamana zinazohitajika na taasisi za fedha.
Kwa mujibu wa Mavunde, mfumo huo utaanza rasmi Julai 1, 2026 kupitia Kampuni ya Credit Guarantee Corporation, ambayo itaanza na mtaji wa kati ya shilingi bilioni 300 hadi trilioni moja kwa ajili ya kusaidia sekta mbalimbali za uzalishaji ikiwemo madini.
Amesema,Serikali pia inaendelea kuwapatia wachimbaji wadogo maeneo rasmi ya uchimbaji na kufuta leseni za maeneo ambayo hayajaendelezwa kwa mujibu wa masharti ya leseni husika.
Waziri Mavunde amesisitiza kuwa,dhamira ya Serikali ni kuwaondoa wachimbaji wadogo katika mfumo wa uchimbaji wa kubahatisha na kuwaingiza katika uchimbaji wa kisasa unaotumia teknolojia, tafiti za kitaalamu na masoko rasmi.
Ameongeza kuwa,Tanzania inalenga kuwa kitovu kikuu cha biashara ya madini barani Afrika kwa kuweka mazingira yatakayowawezesha wachimbaji kupata mitaji ya ndani na kuuza madini yao nchini badala ya kutegemea masoko ya nje.
“Tunataka kuona biashara kubwa ya dhahabu na madini mengine ikifanyika Tanzania. Tukiwapa wachimbaji wetu mitaji na soko la uhakika, tutaimarisha uchumi wa ndani na kuongeza thamani ya madini yetu."
Mfuko na Benki ya Wachimbaji
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu, Dkt.Victor Tesha amesema, utafiti uliofanywa umebaini wachimbaji wadogo bado wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazowakwamisha kufikia uwezo wao kamili wa uzalishaji.
Ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji, matumizi ya teknolojia duni, uhaba wa taarifa za kijiolojia, mazingira hatarishi ya kazi na ukosefu wa mifumo rafiki ya kifedha.
Dkt.Tesha amesema,kamati imependekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Madini Tanzania, ambao utakuwa na jukumu la kusaidia upatikanaji wa fedha za uwekezaji, kugharamia tafiti za kijiolojia, kuwezesha matumizi ya teknolojia bora na kusaidia wachimbaji kuandaa miradi inayoweza kukopesheka.
Pia,amesema baada ya mfuko huo kuimarika, hatua inayofuata itakuwa kuanzishwa kwa Benki ya Wachimbaji, ambayo itatoa huduma maalumu za kifedha zinazozingatia mazingira na mahitaji ya sekta ya madini.
“Kamati imependekeza mikopo ielekezwe zaidi katika ununuzi wa mitambo na teknolojia badala ya fedha taslimu pekee, ili kuongeza tija, uzalishaji na usalama katika shughuli za uchimbaji."
Kwa mujibu wa Dkt.Tesha, sekta ya madini imeendelea kuwa moja ya nguzo kuu za mageuzi ya uchumi wa taifa kutokana na mchango wake katika pato la taifa, ajira, mapato ya Serikali na upatikanaji wa fedha za kigeni.
Amesema,mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023 hadi zaidi ya asilimia 10 mwaka 2024, huku wastani wa asilimia 11.9 ukifikiwa kati ya Januari na Septemba 2025.
Aidha,amesema utafiti wa kamati umeonesha kuwa zaidi ya asilimia 72 ya wachimbaji wadogo bado wanatumia njia za kawaida za uchenjuaji wa madini, hali inayosababisha uzalishaji mdogo na upotevu wa mapato.
FEMATA yaunga mkono mapendekezo
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA),John Bina ameipongeza Serikali kwa kuendelea kusikiliza na kufanyia kazi maoni ya wachimbaji wadogo nchini.
Amesema,ushirikiano uliopo kati ya Serikali na wadau wa sekta ya madini umechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta hiyo na kuongeza matumaini kwa wachimbaji wadogo.
Bina ameitaka Serikali kuunga mkono mpango wa kuanzishwa kwa Benki ya Wachimbaji Tanzania ili kusaidia upatikanaji wa mikopo na mitaji kwa wachimbaji wadogo.
“Ripoti hii ni zao la mawazo, uzoefu na maoni ya wachimbaji pamoja na wataalamu kutoka sekta mbalimbali. Tunaamini mapendekezo yaliyomo yataisaidia Serikali kupanga na kutekeleza mikakati madhubuti ya kuwawezesha wachimbaji wadogo na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya taifa,” alisema.
Serikali yatazamia mageuzi makubwa
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema,mpango huo ni wa kihistoria kwa kuwa unaweka msingi wa maendeleo ya wachimbaji wadogo wa madini kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema, kukamilika kwa ripoti hiyo ni hatua muhimu katika juhudi za kuimarisha sekta ya uchimbaji mdogo wa madini.
Amesema,matarajio ya Serikali ni kuona mapendekezo yaliyowasilishwa yanatumika kama dira ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta hiyo kwa kuongeza tija, uzalishaji na mchango wa wachimbaji wadogo katika uchumi wa taifa.
Kwa ujumla, mapendekezo yaliyowasilishwa yanafungua ukurasa mpya katika historia ya sekta ya madini nchini, yakilenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kupitia mitaji, teknolojia, taarifa za kijiolojia na mifumo rafiki ya kifedha, hatua inayotarajiwa kuongeza ajira, kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi kwa miaka mingi ijayo.
Tags
Anthony Mavunde
Dkt.Victor Tesha
Habari
Prof.Kitila Mkumbo
Wachimbaji Wadogo wa Madini
Wizara ya Madini Tanzania














